NA MWANDISHI WETU, TARIME
BIBI mmoja na wajukuu zake wawili wamefariki baada ya kusombwa na maji wakiwa ndani ya nyumba waliyokuwa wakiishi Mtaa wa Bomani mjini Tarime.
Katika tukio hilo lililotokea Aprili 30, 2023 Saa moja jioni ambapo mbali ya vifo hivyo pia mama na mtoto wake wamenusurika kufa baada ya kusombwa na maji kisha kunasa kwenye mti.
Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mara, Augustino Magere amewataja waliofariki katika tukio hilo ni Ghati Amon (63) na wajukuu zake Vaileth Denis (3) na Johnson Denis (10) ambao walisombwa hadi Mto Bomani uliopo mjini Tarime.
“Baada ya tukio kutokea jana tulianza msako ambapo leo asubuhi tumefanikiwa kuopoa miili yote mitatu kutoka mtoni na miili hiyo hivi sasa imehifadhiwa katika chumba cha maiti kwenye hospitali ya Tarime” amesema
Mwenyekiti wa Mtaa wa Bomani, Chacha Balozi amesema walisikia kelele za kuomba msada na baada ya kufika eneo la tukio walimkuta mama na mtoto wake wakiwa wamenasa kwenye mti.
“Mama huyo alituambia kuwa mama yake mzazi pamoja na watoto wake tayari wamesombwa na maji hadi mtoni tukaanza msako hadi leo tulipofanikwa kuopoa miili yote” amesema
Hata hivyo mwenyekiti huyo amesema kuwa eneo hilo ni hatarishi na tayari walikwishatoa taarifa serikalini ambapo Serikali iliweka vigingi na kuzuia watu kujenga.
“Huyu mama alikuwa ni mpangaji na amehamia hapa wiki tatu zilizopita, mwenye nyumba naye haishi hapa ila alijenga hiki kibanda kwa kiburi maana mwanzoni alizuiliwa baadaye akajenga kama kibanda kwaajili ya ulinzi wa shamba kabla ya kuamua kumpangisha huyu bibi” amesema John Rotete Mkazi wa Mtaa wa Bomani
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Suleiman Mzee amefika katika eneo la tukio na kuwataka wananchi kuwa makini hasa nyakati hizi za mvua.
“DC nakuagiza fanya ufuatiliaji wa haraka na hatua zichukuliwe maana kuna madai kuwa wataalamu wetu walitoa na hati ya kumiliki viwnja hapa jambo ambalo ni kinyume na utaratibu ” amesema
Ameongeza kuwa suala la ulinzi na usalama ni jukumu la kila mtu na kwamba inasikitisha kuona familia hiyo iliamua kuishi katika eneo hilo bila kujali madhara ambayo yangeweza kutokea.
Amemuagiza Mkuu wa Wilaya hiyo, Michael Mtenjele kufanya msako ili kubaini kama kuna watu wanaishi pembezoni mwa mto huo na kuwaondoa kabla hawajapata madhara.