NA DENIS SINKONDE, SONGWE
WATUMISHI sita katika Halmashauri ya Wilaya Ileje mkoani Songwe wamefukuzwa kazi kwa makosa ya utovu nidhamu ikiwemo kutafuna fedha mbichi za makusanyo ya Halmashauri na utoro kazini.
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Ubatizo Songa katika Kikao cha Baraza la Madiwani robo ya tatu kilichofanyika Aprili 29,2023 katika Halmashauri hiyo.
Songa amesema katika orodha ya Watumishi hao sita wanne (4) ni watendaji Kata na vijiji ambao walikiuka kwa makusudi utaratibu wa Halmashauri na kutumia makusanyo ya fedha walizo kusanya huku wakikaidi kuzirudisha fedha hizo.
Songa amesema wengine wawili ni watumishi kada ya afya ambao walilipoti katika vituo vyao vya Kazi kwa zaidi ya miezi mitatu iliyopita, Lakini hadi sasa wananchi wanaendelea kukosa huduma za Watumishi hao kutokana na kutokurudi tena katika vituo vyao vya Kazi.
Mwenyekiti huyo amewataja majina Watumishi hao waliofukuzwa kazi kuwa ni Osward Mwafwongo Mtendaji daraja la pili Kijiji cha Lali ambaye alitumia kiasi cha shilingi 4,751,600, Martin Chonya Mtendaji daraja la pili Kata ya Lupanda alitumia kiasi cha shilingi 6,650,000,
Wengine ni Adili Mkeya Mtendaji daraja la pili Kijiji Cha Ibaba alitumia 5,478,950 na mwingine ni Hussein Sharif Mtendaji daraja la tatu Kijiji Cha Msiya ambaye naye alitumia makusanyo aliyokusanya bila utaratibu.
Kwa upande wa Watumishi wa kada ya afya waliofukuzwa ni pamoja na Emmanuel Mwambije mfamasia aliyekuwa amepangiwa zahanati ya Ibula na Moza Mbaruku mfamasia daraja la pili aliyepangiwa kituo Cha afya Ibaba wilayani hapa.
“Hawa watumishi wa afya waliripoti vituoni na kudai kuwa watarudi baada ya kufuata mizigo yao lakini hadi sasa mmoja amekaa siku 117 bila kuonekana kazini na mwingine siku 193 bila kufanya Kazi sehemu aliyopangiwa kazi , huku wananchi wakiendelea kupata adha ya kupata matibabu
Kwa Mamlaka tuliyopewa hawa wote tunawafuta Kazi kutokana na utovu wa nidhamu wa kuendelea kutumia mishahara ya Serikali pasipo kufanya Kazi ” amesema Mwenyekiti Ubatizo.