NA MWANDISHI WETU, BARIADI
MKUU wa Wilaya ya Bariadi Simon Simalenga ametoa tahadhari kwa Wamiliki wa kampuni zinazonunua Pamba mkoani Simiyu ambayo yanadaiwa na AMCOS na Halmashauri za Mkoa huo kuhakikisha wanalipa madeni hayo haraka iwezekavyo kabla utoaji wa vibali vya kununua Pamba haujaanza vinginevyo hawatapewa vibali vya kununua zao hilo kutokana na baadhi yao kupuuzia ulipaji wa madeni hayo kwa msimu wa 2021/2022.
Simalenga ametoa tahadhari hiyo alipomuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Dkt.Yahaya Nawanda wakati wa ufungaji kwa Jukwaa la III la Ushirika la Mkoa wa Simiyu ambalo awali lilifunguliwa na Mkuu wa Mkoa huo.
Simalenga amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan imefanya jitihada kubwa katika kuleta mbegu za pamba,viuatilifu pamoja na mbolea ili Mkulima aweze kulima kwa tija na kujikomboa kiuchumi na kimaisha, hivyo serikali ya Mkoa wa Simiyu haitakuwa tayari kuona jitihada hizo zikififishwa na mfanyabiashara yeyote kwa kutokulipa madeni hayo na hivyo kujinufaisha wao binafsi jambo ambalo ni kinyume na nia na malengo ya dhati ya . Rais .
Awali Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirikia Mkoa wa Simiyu Godfrey Mpepo alisema moja ya changamoto ni uwepo wa baadhi ya kampuni kutowalipa madeni hayo kwa AMCOS hali ambayo inafifisha jitihada za wakulima kuzalisha zao hilo.