NA MWANDISHI WETU, MALAWI
ZAIDI ya Wafanyabiashara 300 wakiwemo 150 kutoka nchini Tanzania wamejitokeza kushiriki kongamano la biashara na uwekezaji kati ya Malawi na Tanzania lililokuwa na lengo la kufungua fursa za biashara zaidi.
Kongamano hilo ambalo limefanyika kwa siku mbili nchini Malawi liliratibiwa na Wizara ya Uwekezaji Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Ubalozi wa Tanzania nchini Malawi, Kituo cha Uwekezaji (TIC), Taasisi ya Biashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA) na Chama cha Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC).
Akizungumza katika kongamano hilo kwa niaba ya Waziri Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dk. Ashatu Kijaji, Katibu Mkuu wa wizara hiyo Dk. Hashil Abdallah alisema kuwa anawahakikishia wafanyabiashara kupata ushirikiano wa kutosha kwa kuwa mazingira ya biashara yameboreshwa na taasisi zake zote ikiwemo TanTrade ambayo ipo tayari kutoa mwongozo na taarifa kuwezesha mauzo ya nje.
Alisema Tanzania inawakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara kutoka Malawi kuja kuwekeza na kufanya biashara nchini hasa katika sekta za kilimo, uvuvi, uchumi wa bluu, uzalishaji utalii, huduma za fedha, uchukuzi, miundombinu, mawasiliano, madini elimu na afya ili kukuza biashara na uchumi wa nchi hizo mbili.
“Wafanyabishara na wawekezaji wa Tanzania tumieni kikamilifu fursa zinazopatikana baina ya nchi hizi mbili kulingana na rasilimali zilizopo ili kuongeza kasi ya ukuaji wa biashara ambayo imefikia kiasi cha dola za Marekani Milioni 86.7 mwaka 2022,” alisema Dk. Abdallah
Naye Waziri wa Viwanda na Biashara wa Malawi, Simplex Banda amekitaka Kituo cha Biashara Malawi kushirikiana na Tanzania kuandaa kongamano kila baada ya muda mfupi tofauti na kipindi cha miaka mitano tangu lifanyike la kwanza upande wa Tanzania.
Pia Waziri Banda aliwasilisha shukrani kwa niaba ya Rais wa Malawi Lazarus Chakwera
ambapo amemshukuru Rais wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan kwa msaada wa chakula na vifaa vya kujihifadhi aliyoutoa wakati Malawi ilipokumbwa na kimbunga freddy mapema Machi 2023.
Kwa upande wa Balozi Mteule wa Tanzania Nchini Cuba ambaye alikuwa akiiwakilisha Tanzania nchini Malawi, Balozi Humphrey Hezron Polepole alisema kongamano hilo limewakutanisha wafanyabiashara na wawekezaji kujadili na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili katika biashara zao baina ya nchi hizo.
Aidha aliwashauri watanzania kuwa wabunifu na kushirikiana na wafanyabiashara wa Malawi kutumia fursa za biashara na uwekezaji zilizopo nchini Malawi ambayo ni moja ya nchi sisizokuwa na bahari.
Tanzania na Malawi zimekubaliana kukuza uhusiano wa kibiashara na uwekezaji kwa kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji baina ya nchi hizo ikiwemo uboreshaji wa sheria za uwekezaji, ukamilishaji wa ujenzi wa kituo cha pamoja cha Kasumulo na huduma za Bandari ya Mbamba Bay ili kukuza biashara na uchumi.
Hata hivyo kama sehemu muhimu ya kuhitimisha Kongamano hilo,TanTrade ilishirikiana na Taasisi ya Biashara Malawi (MTC) kuwatembeza Wafanyabiashara katika kiwanda cha Kwithu Kitchen na pia shamba la zao la Makademia (hekta 2000) la kampuni ya Tropha Mzuzu kujifunza kwa vitendo kuhusu uzalishaji na uongezaji thamani pamoja na biashara za kimataifa.