NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema kinataka kufanya siasa za kisasa zitakazobadilisha mwelekeo wa nchi kupitia mila na desturi za Kitanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari Aprili 28, 2023 mkoani Dar es Salaam, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Sophia Mjema alisema kuwa wamejifunza mambo mbalimbali walipokuwa nchini China ikiwemo elimu na ufundi stadi, habari na mawasiliano, kilimo, uvuvi, afya na viwanda.
Alisema kuwa China imeweza kufanikiwa kupitia majimbo matatu na kwamba Tanzania ina nafasi ya kufanya mapinduzi ya kimaendeleo sambamba na kuondoa umasikini.
“Tunampongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufungua milango ya mahusiano na ushirikiano kimataifa, kwani ziara hii imekuwa na mafanikio makubwa yatakayokuwa chachu ya kuendelea kuchagiza na kudumisha uhusiano katika nyanja mbalimbali kwa maslahi ya vyama vyetu na wananchi wa nchi zetu mbili,” alisema Mjema.
Alieleza kuwa ziara ya Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo na wajumbe 20 wa Halmashauri Kuu na wataalamu wawili wa chama hicho, ni utekelezaji wa makubaliano na maelekezo yaliyotolewa na viongozi wakuu, yaani Rais Samia na Katibu wa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Xi Jinping.
Alisema viongozi hao walikubaliana kupandisha hadhi ya uhusiano kati ya CCM na CPC, kati ya Tanzania na China kwa kuwa na uhusiano maalumu wa kimkakati katika nyanja za elimu na ufundi stadi, habari na mawasiliano, kilimo, uvuvi, afya na viwanda.
Mjema alisema kupitia ziara hiyo wamejifunza na kuona jinsi wenzao walivyofungua nchi kiuchumi kupitia majimbo ya Shengzen, Guandong na Guanzhou.
“Aprili 17 hadi 28, mwaka huu, Chongolo na ujumbe wake walitembelea majimbo matatu nchini China ambayo ni Shengzen, Guandong na Guanzhou katika ziara hiyo, walikutana na kufanya mazungumzo na viongozi mbalimbali wa CPC, Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China ambao ni Mkurugenzi wa Kamisheni ya Mambo ya Nje wa Kamati Kuu ya chama hicho, Wang Yi, Waziri wa Idara wa Mambo ya Nje, Liu Jianchao, wengine ni Naibu Waziri wa Idara ya Mambo ya nje, Li Mingxiang, Katibu wa chama hicho jimbo la Hebei, Ni Yuefeng na Mjumbe wa Kamati ya kudumu ya CPC jimbo la Guandong, Wang Ruijun,’’ alifafanua.
Mjema alisisitiza kuwa kupitia ziara hiyo kama nchi imefungua fursa za uwekezaji na kufanikisha dhana ya serikali ya China ya kuja kufungua uchumi Afrika.
“Kwa ujumla ziara hii imekuwa na umuhimu katika kuboresha na kuimarisha mahusiano ya CCM na CPC. Nawataka wanachama na viongozi wa CCM na Watanzania kwa ujumla kuchangamkia fursa zitokanazo na matunda ya ziara hii,’’ alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida, Martha Mlata alisema walichojifunza China ni jinsi nchi hiyo ilivyowawezesha vijana kufanya kazi na kujiajiri maeneo mbalimbali.
“China wanayo misimamo ya pamoja kiujamaa ulio maalumu kwa nchi yao, hivyo sisi tuwe na ujamaa maalumu kwa Tanzania kwa sababu wanachoamua ndicho wanachokifanya,” alisema Mlata.