NA MWANDISHI WETU, MANYARA
MAHAKAMA ya Wilaya ya Babati mkoani Manyara imemhukumu mkazi wa Kijiji cha Gendi , Issaya Mtinangi (35) kifungo cha miaka 30 jela kwa kumbaka mfanyakazi wa ndani (15).
Hukumu hiyo imetolewa mjini Babati na Hakimu mfawidhi wa mahakama hiyo Victor Kimario.
Amesema mshtakiwa ametenda kosa hilo Desemba 15 mwaka 2022, Kijiji cha Gendi ambapo alidai alifanya mapenzi na binti wa miaka 15 bila ridhaa yake.
Hakimu amesema shahidi namba moja ambaye ndio mwathirika amedai mahakamani hapo kuwa Mtinangi ndiyo alimtafutia kazi ya ndani binti huyo ambapo alimtoa Katesh akiwa na mwenzake na kuwashusha jirani na ofisi za Tanesco na mara baada ya kuwashusha binti huyo alimpeleka Mtaa wa Ngarenaro Babati Mjini na kumkabidhi kwa mama Amina amfanyie kazi.
Amesema mshtakiwa alikiuka kifungu cha 130 (1) (2) (e) na kifungu cha 131 (1) cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.
Amedai siku ya tukio mshtakiwa alikwenda kwenye familia ya binti huyo alipokuwa anafanya kazi na kuwaambia kuna ndugu zake wanamhitaji ili aende awaone ndugu zake lakini kumbe alikuwa na nia ovu ambapo alimpeleka nyumbani kwake Gendi na kumlazimisha kufanya mapenzi.
Kimario amesema mahakamani hapo kuwa alimuingilia mara mbili na baada ya unyama huo alimuamuru kupika ugali hivyo wakati anapika ugali mshtakiwa alipitiwa na usingizi na binti akapata nafasi ya kukimbia akipiga kelele kuwa amebakwa akasaidiwa na baadhi ya watu wema kwenda polisi.
Kimario amedai kuwa Mahakama imemtia hatiani mshtakiwa baada ya upande wa mashtaka kupeleka mashahidi wanne ambao walitoa ushahidi usioacha shaka juu ya mshtakiwa na Mtinangi alijitetea mwenyewe.
Vile vile amedai kuwa kwa mujibu wa vipimo vya daktari vimeonesha kuwa binti huyo alibakwa baada ya kukutwa na mbegu za kiume.
Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Emmanuel Jumbe kabla ya kutolewa hukumu hiyo amesema mshtakiwa hana kumbukumbu za makosa ya nyuma hivyo Mahakama itoe adhabu kali ili iwe fundisho kwa jamii.
Kwa upande wake Mtinangi alipopewa nafasi ya kujitetea ameiomba mahakama imwangalie kwa jicho la huruma kwani mama yake amezeeka na anamtegemea lakini analea mtoto wa dada yake ambaye alishatangulia mbele ya haki.