NA MWANDISHI WETU, SENGEREMA
WAKALA wa Barabara Tanzania (Tanroad) leo Aprili 23, 2023 imetia saini ya mkataba wa ujenzi wa barabara ya Sengerema-Nyehunge yenye urefu wa Kilometa 54.4 na kampuni ya AVM-Dilingham ya nchini Uturuki.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanroad, Rogatus Mativila amesema barabara hiyo inayojengwa kwa gharama ya Sh.Bil 73.04 kwa muda wa miezi 28 inatarajia kuchochea shughuli za kiuchumi na kuunganisha mikoa ya kanda ya ziwa.
“Barabara hii itakapokamilika itachochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi kama vile usafirishaji wa mazao ya misitu, mazao ya chakula, mazao ya uvuvi pamoja na mazao ya biashara na shughuli za kijamii kwa ujumla,” amesema.
“Mradi wa Ujenzi wa barabara ya Sengerema hadi Nyehunge ni moja ya mikakati ya Serikali ya kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii mkoani Mwanza hususan katika wilaya ya Sengerema kwa kuboresha mtandao wa barabara ili kuongeza ufanisi katika sekta ya usafiri na usafirishaji,”ameongeza.
Kwa upande wake, Mbunge wa Sengerema, Hamis Tabasamu amesema kujengwa kwa barabara hii Kwa kiwango cha lami kutaleta fursa mbalimbali kwa wananchi wa eneo hilo.
“Ninamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutimiza ahadi iliyoachwa na Hayati John Magufuli (Rais wa awamu ya tano) kuhusu kujengwa barabara hii Kwa kiwango cha lami,” amesema Tabasamu.
Amos John, mkazi wa Sengerema amesema ukamilishaji wa barabara hiyo utaenda kutoa fursa za ajira kwa vijana na kujiajiri.
“Barabara hii inakwenda kufungua fursa za biashara kwetu na mazingira wezeshi ya kujiajiri, hivyo wananchi tunapaswa kuitunza miundombinu yake,”amesema.