NA MWANDISHI WETU, MWANZA
MKAZI wa Mtaa wa Bwiru Msikitini Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza, Emmanuel Nyambera (40) amefariki dunia kwa kujipiga risasi kifuani kwa kile ambacho uchunguzi wa awali wa Jeshi la Polisi umebaini kuwa ni kukwepa mgogoro wa mgawanyo wa mali.
Akizungumza na waandishi wa habari Aprili 21, 2023, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa amesema marehemu ambaye wakati wa uhai wake alijihusisha na shughuli za kibiashara alijipiga Saa 3:45 usiku wa Aprili 16 mwaka huu.
Ametaja silaha iliyotumika katika tukio hilo ni bastola aina ya Charter ambayo ilikuwa ikimilikiwa kihalali na marehemu wakati wa uhai wake.
Kamanda Mutafungwa amesema katika mahojiano, jeshi la Polisi limebaini kabla ya kujitoa uhai kwa kujipiga risasi, Nyambera anayemiliki biashara na mali kadhaa maeneo tofauti nchini ikiwemo Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga alioa mke wa pili ambaye alimjengea nyumba na kumfungulia biashara kadhaa wilayani humo.
“Familia ya mke mkubwa ilipobaini kuwa kuna mwanamke mwingine ikaanza kutoa shinikizo la kufanyika kwa mgawanyo mali kutoa fursa ya kila upande kupata haki na huduma stahiki. Shinikizo hilo lilisababishia msongo wa mawazo baba wa familia ambaye alifikia uamuzi wa kujiua kwa kujifyatulia risasi kifuani,” amesema Kamanda Mutafungwa
Amesema mwili wa marehemu tayari umekabidhiwa kwa familia kwa ajili ya mazishi baada ya uchunguzi na mahojiano na mashuhuda mbalimbali kuhusu tukio hilo kukamilika.
“Jeshi la Polisi linawasihi wananchi wenye ama matatizo au jambo lolote linalowasumbua kushirikisha ndugu, jamaa, wanasaikolojia, viongozi wa kidini na kijamii au watu wanaowaamini kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi badala ya kuchukua hatua na maamuzi yanayoweza kusababisha madhara,” amesema na kushauri Kamanda Mutafungwa
Akizungumzia tukio hilo, Mkazi wa Mahina jijini Mwanza, Sophia Juma amewashauri wanandoa kutumia njia ya majadiliano na mashauriano kutatua matatizo yanayowakabili badala ya kuchukua uamuzi unaoweza kusababisha madhara kwao wenyewe au watu wengine.