NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
SHIRIKA la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limetoa notisi ya miezi mitatu kwa wananchi waliosaini mikataba ya fidia kupisha mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika ya Mashariki (EACOP).
TPDC imeagiza kuwa kuanzia Mei Mosi hadi Julai 31, mwaka huu wananchi wawe wameondoka kwenye maeneo na kuwa mradi utatoa usaidizi wa kuwahamisha kwenda maeneo ya karibu.
Aidha, kaya zilizoguswa makazi yao ambazo zilichagua fidia ya fedha taslimu zinapaswa ziwe zimeondoka kwenye nyumba au ardhi zilizoguswa na mradi itakapofika Julai 31, mwaka huu.
Kadhalika, kaya zilizochagua fidia ya nyumba mbadala zitaondoka kwenye ardhi ya mradi mara tu baada ya ujenzi wa nyumba zao kukamilika na wao kuhamishwa kwenye makazi yao mapya.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Aprili17, 2023 na Kampuni ya Mradi wa EACOP, waguswa wote wanaruhusiwa kutumia ardhi zao hadi tarehe ya mwisho ya kuondoka lakini hawaruhusiwi kupanda mazao ya kudumu au miti, kujenga majengo mapya au kuboresha yaliyopo.
Aidha, taarifa hiyo inakataza pia shughuli zote za maziko kufanywa katika maeneo hayo yaliyopitiwa na mradi kwa sababu hakuna fidia ya nyongeza itakayotolewa kwa mazao au matumizi mengine ya ardhi katika kipindi hicho.
“Kaya zilizoguswa makazi ambazo zilichagua fidia ya fedha taslimu zinapaswa ziwe zimeondoka katika eneo hilo ifikapo Julai 31, mwaka huu kwa sababu waguswa wote waliosaini mikataba yao ya fidia, wamepokea malipo yao ya fidia isipokua kaya chache zinazoguswa makazi ambazo zilichagua fidia ya nyumba mbadala.
Ujenzi wa nyumba zao unaendelea na zitakabidhiwa kwao mara tu baada ya kukamilika,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Taarifa hiyo inawakumbusha waguswa wote kuwa ardhi na makazi katika maeneo ya miundombinu ya juu na barabara zake ambao walipokea notisi Februari 6, mwaka huu za kuondoka wanatakiwa kuondoka kwenye ardhi hizi ifikapo Mei 6, mwaka huu.