NA MWANDISHI WETU, DODOMA
SERIKALI imelipa Sh bilioni 25.7 ambazo ni madai ya malimbikizo ya mishahara kwa watumishi 14,398 hadi mwezi Machi mwaka huu.
Pia imelipa Sh bilioni 8.5 ambazo ni madai ya malimbikizo ya mishahara kwa watumishi 2,942 waliokoma utumishi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene amesema hayo bungeni Dodoma Aprili 19, 2023 wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2023/2024.
Simbachawene amesema katika kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Februari mwaka juzi hadi Machi mwaka huu, Serikali ya Awamu ya Sita imelipa madai ya malimbikizo ya mishahara kwa watumishi 119,098 yenye thamani ya Sh bilioni 204.4.
Pia amesema vibali vya ajira mpya 30,000 na vibali vya ajira mbadala 7,721 kwa waajiri kutoka katika taasisi mbalimbali vilitolewa pamoja na uhakiki uliofanyika kupitia mfumo wa taarifa za kiutumishi na mishahara watumishi wa umma kwa waajiri 380 kati ya waajiri wote 433 kwa lengo la kuboresha huduma na maslahi ya watumishi.
“Pia serikali imeandaa mfumo wa tathmini ya mahitaji ya watumishi wa umma unaowezesha kubaini idadi ya watumishi waliopo, kada zao, nafasi ya kazi, vituo vya kazi na majukumu wanayotekeleza ili kubaini mahitaji halisi, upungufu au ziada ya watumishi katika taasisi za umma kwa ajili ya kuchukua hatua,” amesema Simbachawene.
Ameongeza: “Hadi sasa waajiri wote wamejaza taarifa muhimu katika mfumo; mfumo umewezesha kubaini watumishi waliopo wa kada ya walimu 256,479, kati ya hao, walimu wa msingi ni 171,920 na sekondari ni 84,559.
“Pia mfumo umebaini mahitaji ya walimu nchi nzima lakini pia mfumo huo umetengenezewa moduli inayofanya uchambuzi wa kada nyingine na kazi ya uchambuzi inaendelea.”
Aidha, amesema kwa mujibu wa utafiti wa hali ya uadilifu katika utumishi wa umma uliofanyika mwaka jana, umebainisha kuwa kiwango cha uadilifu katika utumishi wa umma kimeongezeka hadi kufikia asilimia 75.9 ikilinganishwa na asilimia 66.1 mwaka 2014.