NA MWANDISHI WETU, ZANZIBAR
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi amewaomba sekta binafsi Zanzibar kuwalipa mishahara watumishi wao wa sekta hizo leo na kesho kabla ya Sikukuu ya Idd.
Ameyasema hayo leo Aprili 19, 2023 katika fainali za mashindano ya Quran kwa njia ya Tar-til yaliyoandaliwa na Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) kwa kushirikiana na ofisi ya Mufti Mkuu Zanzibar yaliyofanyika ukumbi wa Golden Tulip Airport, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Aidha Dk Mwinyi amewakumbusha wazazi na walezi katika kipindi hiki cha sasa kukabiliana na vitendo vya mmong’onyoko wa maadili kwa kuwaweka karibu watoto na kusimamia nyendo zao katika kuwaandaa vijana kuwa raia wema na wenye hofu kwa Mwenyezi Mungu.
Rais Dk Mwinyi amekabidhi zawadi kwa mshindi wa kwanza Said Juma kutoka Mkoa wa Mjini Magharibi gari aina ya Toyota Alphard , mshindi wa pili Nassor Kombo alipewa zawadi ya pikipiki na mshindi wa tatu Zakaria Shehaalikabdhiwa Sh milioni mbili . Pia Rais Dk Mwinyi ametoa Sh milioni tano kwa mshindi wa nne mpaka wa nane wa fainali hizo.