NA MWANDISHI WETU, IRINGA
BODI ya Tumbaku Tanzania (TTB), imewaagiza wakulima wa tumbaku katika maeneo yote yanayozalisha zao hilo nchini kutouza zao hilo la kimkakati kwa kampuni zisizo na leseni za kununua bidhaa hiyo.
Hayo yanebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji TTB Stanley Mnozya. kwenye mkutano wa wadau wa tumbaku uliofanyika mjini Iringa na kujadili changamoto na upangaji wa madaraja ya tambaku.
“Wakulima msiuze tumbaku kwa makampuni ambayo hayana leseni ya kununua tumbaku kutoka TTB na bodi itatoa maelekezo haya kwa wakulima wote nchini,” amesema Mnozya.
Mnozya amezitaka kampuni zilizopata leseni za kununua malighafi hiyo inayotumika kutengenezea sigara kupitia vyama vya ushirika.
“Bodi imetoa leseni za ununuzi kwa baadhi ya kampuni na zipo kampuni nyingine ziliomba leseni, lakini hazikupata, kampuni hizo zitambue zimekosa leseni kwa sababu hazijakidhi vigezo hivyo, wakulima wasiuze tumbaku kwao,” amesema.
Pia amewaomba wakulima kuhakikisha wanang’oa mabua ya tumbaku mashambani, kabla ya kuanza masoko na kuongeza kuwa vyama vya msingi ambavyo wakulima wake hawatatekeleza agizo hilo masoko yao hayataanza.
Amesema hatua ya kung’oa mabua inalenga kupuungza wadudu na usugu wa magonjwa kwa zao hilo.
Mnozya amesema tumbaku ni zao la serikali la kimkakati linalochangia kwa kiasi kikubwa fedha za kigeni na pato la taifa.
Ameiomba serikali kupitia mfumo wake wa usambazaji pemebejeo kwa wakulima uwe kwa wakati, ili kuwawezesha kuzalisha kwa tija.
TTB pia imewataka wakulima na wadau mbalimbali wa tumbaku kuendelea kupanda miti kwa wingi, ili kulinda mazingira, kwani ukaushaji wa tumbaku unatumia zaidi nishati ya kuni.
Akifungua mkutano huo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa Halima Dendego amewataka wanunuzi wa zao hilo kufanya biashara kistaraabu na kizalendo kwa kununua kwa bei inayoendena na masoko ya kimataifa ili wakulima nao wapate faida.
Amesema zipo kampuni yanayolalamikiwa sana na wakulima kuwanyonya kwa kununua zao hilo kwa bei ndogo ambayo aiendani na soko.
Amesema wanunuziwakinunua tumbaku kwa bei nzuri itawafanya wakulima waeendelee kuwa na moyo wa kuzalisha kwa tija na kwa wingi zaidi.
“Wanunuzi msiwakatishe tamaa wakulima, wakulima wakiacha kuzalisha kwa sababu ya bei ndogo hiyo ni hasara kwa kampuni zenu, viwanda na ni changamoto kwa ajira za watu wetu,” amesema.
Amesema ili kuwepo na uzalishaji endelevu wa tambaku, lazima mnyororo wa thamani wa zao hilo uwekewe msukumo mpya na akawataka wataalamu na maofisa kilimo mkoani humo kufuatilia uzalishaji wake ili kuweza kuuweka mkoa katika ramani.
Pia Dendego amewataka wakulima mkoani Iringa kuongeza uzalishaji wa zao hilo kama mikoa mingine akisema takwimu zinaonesha ni wa mwisho kwa uzalishaji pamoja na uwepo wa ardhi ya kutosha na hali ya hewa nzuri.
Mbali na Iringa mikoa mingine inayozalisha tambaku ni pamoja na Ruvuma, Katavi, Mbeya, Tabora, Kigoma, Shinyanga, Singida, Mara, Geita, Kagera na Morogoro.
Mara ya mwisho mkutano kama huo ulifanyika mwaka 2011.