NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
TAASISI na mashirika ya umma yanayojiendesha kibiashara yametakiwa kuhakikisha yanajiendesha yenyewe kwa faida wanazozipata, lengo likiwa kupunguza utegemezi kutoka serikalini.
Hayo yamesemwa leo Aprili 19, 2023 na Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu, katika mkutano wake na Wenyeviti wa Bodi pamoja na Watendaji Wakuu wa taasisi, mashirika ya umma na wakala za serikali uliofanyika ukumbi wa mikutano wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.
“Tulichonacho sisi tunapaswa kutoa msaada kama wadau, kwa maana tabia, ufikiri na matendo kuanzia mimi mwenyewe na timu yangu yote, tunapaswa kuwa na mtizamo wa kibiashara. Hii ni hata taasisi za elimu ambao tunakutana nao kesho. Lengo ni kupunguza utegemezi,” amesema Mchechu.
Amezitaja baadhi ya taasisi zinazotoa huduma za kibiashara kuwa ni DAWASA, ambapo amesema kuwa taasisi hizo zina muunganiko wa utoaji huduma na biashara na ndiyo maana wanatengeneza kipato cha ziada.
“Tanga UWASA, kwa mfano, wapo kwenye hatua za kutoa bondi yao. matumizi ya ile bondi ni miundombinu kwa asilimia 80. taasisi hii imeweza kutengeneza kipato cha ziada, na kwa kiasi kikubwa itaipunguzia serikali mzigo wa gharama za miundombinu,” ameongeza Mchechu.