NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
ALIYEWAHI kuwa Mbunge wa Butiama mkoani Mara, Nimrod Mkono amefariki dunia akiwa nchini Marekani alipokuwa akitibiwa tangu mwaka 2018.
Kwa mujibu wa mdogo wa Marehemu, Zadock Mkono amethibitisha kutokea kwa kifo hicho akisema kimetokea leo Aprili 17 Florida nchini Marekani.
“Taarifa ni za kweli, hata mimi nimezungumza na binti yake na mkewe wamesema kuwa amefariki leo (jana) saa za aubuhi huko Amerika. Alikuwa anatibiwa nchini Marekani katika jimbo la Florida miaka minne iliyopita ,” amesema.
Amesema Mkono alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu (Alzheimer).
“Nimeongea na ndugu kule wanasema mwili utaletwa kuzikwa Tanzania, japo utachelewa,” amesema.
Mkono, aliyezaliwa Agosti 18, 1948, Busegwe Mkoani Mara alikuwa mwanasheria na mwanasiasa maarufu.
Akizungumzia msiba huo, Mwenyekiti mstaafu wa CCM Mkoa wa Mara, Samuel Kiboye maarufu Namba tatu amesema kuwa chama hicho kimepoteza kada mtiifu na mpenda maendeleo wa kweli.
Kiboye amesema kuwa katika kipindi chake cha ubunge Mkono alifanya mambo mengi ya kimaendeleo katika sekta mbambali ikiwemo sekta ya elimu.
“Mkono amejenga shule za kisasa kule Butiama na hadi sasa wapo wanafunzi wanasoma na hata pale kilipo chuo kikuu cha Mwalimu Julius Nyerere cha Kilimo na Teknolojia ni shule aliyojenga yeye,” amesema.
Amesema kwa ushiriki wa Mkono katika maendeleo ya chama pia haukuwa wa wasiwasi kwani ameshiriki mambo mengi ya kimaendeleo ya chama hicho kaunzia ngazi ya wilaya hadi mkoa.
“Ofisi za CCM mkoa kwa sasa zipo kwenye jengo alilojenga Mkono kwa pesa yake mwenyewe, lakini pia ni miongoni mwa watu waliofanikisha harambee ya chama chetu mwaka 2005 vile vile ametoa michango ya fedha taslimu kwa jumuiya za chama kwaajili ya maendeleo,” amesema.