NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM.
TAASISI ya Elimu Tanzania (TET) imefanya uzinduzi wa Maabara ya Tehama kwa shule ya Msingi Tegeta ‘A’ ya jijini Dar es salaam sambamba na kukabidhi vifaa vya Kielektroniki kutoka nchini Korea kupitia mradi wa KLIC 2022 (Korean e-learning Improvement Cooperation 2022).
KLIC 2022 ni programu ya mafunzo yaliyotolewa na nchi ya Korea kwa kushirikiana na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kwa njia ya mtandao kwa Walimu 20 wa shule ya Msingi Tegeta A.
Akikabidhi vifaa hivyo leo Aprili 18, 2023 Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dk.Aneth Komba amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha sekta ya Elimu nchini ambapo ameeleza kuwa walimu katika shule hiyo wataweza kutekeleza kwa urahisi kazi ya ufundishaji na ujifunzaji kwa njia ya kieletroniki.
Dk.Komba amewataka walimu hao kuhakikisha wanaleta matokeo chanya ambayo yatasaidia katika uboreshaji wa elimu.
“Mkayatumie mafunzo vizuri na vifaa hivyo mlivyokabidhiwa kwa kuleta matokeo chanya na tuone ongezeko la ufaulu kwa wanafunzi wa Tegeta A”, Amesema Dkt.Komba.
Tukio hilo liliambatana na kukabidhi vishikwambi 20 kwa walimu walioshiriki programu ya mafunzo hayo.
Kwa upande wake , Mwalimu Mkuu wa shule ya Tegeta ‘A’, Alistides Ntakire ameshukuru kwa mafunzo hayo pamoja na vifaa vilivyotolewa ambapo amesema ana imani yataleta tija katika shule yake.
Naye Mwenyekiti wa kamati ya shule hiyo, Yassin Marijan ameshukuru kwa kuzinduliwa maabara hiyo ya Tehama na kukabidhiwa vifaa vyote huku akieleza kuwa atahakikisha vinatumika ipasavyo katika kuboresha elimu.
Vifaa vilivyokabidhiwa ni pamoja na kompyuta 25, keyboard 35, projekta 1, Skana moja, printa moja,flashi diski 50 , spika 26 na vifaa vingine vingi.


Baaadhi Walimu wa shule ya Msingi Tegeta ‘A wakiwa wamebeba vifaa vya kielektroniki vilivyotelewa na Korea kupitia mradi wa KLIC 2022, leo Aprili 18, 2023.

Mkrugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dk Aneth Komba akiwa anavitoa kuwakabidhi vifaa vya kielektroniki vilivyotelewa na Korea kupitia mradi wa KLIC 2022 uongozi wa shule ya Tegeta A, kulia kwake ni Mkurugenzi wa Mafunzo ya Mitaala, Dk.Fika Mwakabungu.Makabidhiano hayo yamefanyika leo Aprili 18, 2023.

Mkrugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dk.Aneth Komba akikamkabidhi Mwalimu Mkuu wa shule ya Tegeta A, Mwalimu Alistides Ntakire vifaa vya kielektroniki vilivyotolewa na Korea kupitia mradi wa KLIC 2022 leo Aprili 18,2023.

Mkrugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dk.Aneth Komba akikata utepe kuashiria kuzindua rasmi Maabara ya TEHAMA katika shule ya Msingi Tegeta ‘A’ Kulia kwake ni Mwenyekiti wa Kamati ya Shule, Yassin Marjan leo Aprili 18, 2023.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dk.Aneth Komba akizungumza katika tukio la kukabidhi vifaa vya kielektroniki vilivyotolewa na Korea kupitia mradi wa KLIC 2022 na uzinduzi wa Maabara ya TEHAMA leo Aprili 18, 2023.