NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
RAIS wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan ameema kuwa tani milioni 18.5 zenye asilimia 4.5 ya madini adimu zimegundulika kuwepo katika Kijiji cha Ngwala wilayani Songwe na kwamba madini hayo yatachimbwa kwa zaidi ya miaka 20.
Rais Dk Samia ametoa kauli hiyo leo Ikulu Chamwino mkoani Dodoma mara baada ya kushuhudia utiaji saini wa mikataba ya makubaliano kati ya Serikali na kampuni tatu za madini kutoka Perth nchini Australia.
Kampuni hizo zinakwenda kuchimba madini katika vijiji vya Epanko (Morogoro) ambapo yatachimbwa madini ya Kinywe Chilalo (Lindi) yatachimbwa madini ya kinywe pia huku Ngwala (Songwe) ndio madini hayo adimu yatachimbwa.
Amesema utafiti ulioanza kufanyika katika maeneo hayo mwaka 2000 umebaini kuwa katika Kijiji hicho cha Ngwala kuna madini adimu na kwamba yatachimbwa kwa muda wa zaidi ya miaka 20.
“Katika Kijiji cha Chilalo kuna mashapo yenye tani milioni 67 zenye wastani wa asilimia 5.4 za madini ya Kinywe ambayo yatachimbwa kwa muda wa zaidi ya miaka 18 na katika Kijiji cha Epanko kuna mashapo yenye tani milioni 63 zenye wastani wa asilimia 7.6 za madini ya Kinywe nayo yatachimbwa kwa muda wa zaidi ya miaka 18,” amesema na kuongeza
“Kuna maeneo ambayo zamani kulikuwa tunaamini ni masikini hayana rutuba wala vyanzo vingine vya fedha kumbe Mungu ameficha mali, sasa tumejua kwamba ni mali hivyo maeneo hayo yanakwenda kunyanyuka,” amesema
Mkoa wa Lindi na Morogoro ipo katika ukanda wa madini Kinywe na mkoa wa Songwe upo katika ukanda wenye madini adimu ‘rare earth element’ ndio maana miradi hii ipo Chilalo (Lindi), Epanko wilayani Ulanga na Ngwala wilayani Songwe,” amesisitiza Rais Dk. Samia.
Aidha Rais Dk. Samia amewataka wakazi wa mikoa ya Lindi, Morogoro na Songwe kuchangamkia fursa ya uweo wa miradi ya uchimbaji madini katika mikoa hiyo ili kuweza kujiletea maendeleo.
Amesema ni muhimu watanzania wakajipanga kwa kufanya kazi kwa bidii katika mikoa hiyo ambayo madini yamegundulika hasa kwa kufanya kazi ya mama lishe, uuzaji wa vinywaji kama soda na maji.
Pia amewataka wawekezaji wanaotumia fedha za miradi kama fursa za kujikuza kiuchumi kuacha mara moja kufanya hivyo kwani mambo hayo yana uhujumu uchumi.
“Tuna mtindo ndugu zangu wawekezaji tunachukua miradi na kwenda kuweka ‘deposit’ zetu kwenye ‘stock exchange’ tunagenerate fedha kwanza alafu ndio tunarudi kuwekeza bila kujali kwamba huu ni uhujumu uchumi kwa nchi yetu,” amesema