NA MWANDISHI WETU, SINGIDA
BAADHI ya matajiri wanadaiwa kuwezesha mauaji ya watu, wizi wa vitu na viungo vya maiti vinavyofanywa na wanaofukua makaburi, wilayani Manyoni katika Mkoa wa Singida.
Hayo yamebainika baada ya mahojiano kati ya Jeshi la Polisi na watuhumiwa ambao wanaendelea kukamatwa, katika operesheni inayofanywa na jeshi hilo katika Mkoa wa Singida, kufuatia kuibuka aina hiyo ya uhalifu hivi karibuni.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida, Stella Mutabihirwa, amesema hayo akizungumza na vyombo vya habari mjini Singida, kwamba wanafanya hayo kwa kuwa na imani potofu za kishirikina.
“Imeonesha wanatumwa na baadhi ya matajiri wanaotaka kulinda utajiri wao au kupata utajiri, imani ambayo ni potofu,” amesema Kamanda Mutabihirwa.
Amesema imani hiyo potofu inatokana na wafanyabiashara hao kushiriki ramli chonganishi zinazofanywa na waganga wa jadi walaghai, ambao huwaagiza kupeleka viungo vya watu na viambata vya maiti, ambavyo hupatikana kwa kufukua makaburi.
Amesema matajiri hao wamekuwa wakiaminishwa kwamba vitu hivyo vinapofanyiwa uganga, hupatikana dawa za kuendeleza au kupata utajiri, imani isiyo kweli.
Amesema hadi Ijumaa wiki hii operesheni hiyo ilikuwa imewakamata watu 13, wakihusishwa na uhalifu huo.