KIAMBU, KENYA
FAMILIA moja kutoka kaunti ya Kiambu nchini Kenya imeitaka hospitali kuuzika mwili wa mpendwa wao baada ya kushindwa kupata kiwango cha fedha walizokuwa wakidaiwa kama bili ya matibabu
Familia inaitaka hospitali kuzika mwili wa mpendwa wao baada ya kushindwa kulipa bili yake.
Familia hiyo iliyopo Kabete inadaiwa bili ya shilingi takribani milioni moja ili kuruhusiwa kuuchukua mwili wa mpendwa wao japo wao wanasema kuwa wamejaliwa kupata 40,000 kupitia michango waliofanya.
Marehehemu aliyefahamika kama Leston Kinuthia alifariki mwezi mmoja uliopita na familia imekosa kupata kiwango kinachohitajika kuutoa mwili wake hospitalini.
Kulingana na baba wa marehemu Kinuthia , Tilas Wangati ambaye amesema kuwa hana njia yeyote ya kulipa bili hiyo ya hospitali amedokeza kuwa waliwasilisha shilingi 40,000 walizopata katika ili wauchukue mwili wa marehemu lakini hospitali imewakatalia kuwapa mpendwa wao hadi pale deni hilo litakapomalizika kulipwa.
“Nilipewa bili ya shilingi 945,000 na nikaona siwezi kulipa hiyo kwa sababu sina kazi sina kitu ambacho ninaweza kuuza. Kwa hivyo nimekata kauli mimi na watoto wangu tunauliza serikali inaweza kutusaidia wazike huyo mtoto wangu,”amesema Wangati
Dada wa marehemu Kinuthia , Rosebel Wairimu amesema kuwa ombi lao la kutaka kumzika mpendwa wao halikuwezekana kwani hospitali ilihitaji angalau theluthi tatu ya pesa ambazo walikuwa wanadaiwa.
“Tulitafuta pesa na tukajaliwa kupata 40,000 ambayo haikutusaidia. Tulivyoenda huko kuomba watusaidie walituambia hawawezi na kuwa tulihitajika kutoa angalau theluthi tatu ya pesa na kisha twende na kitu kitakachoonesha kuwa tutakamilisha kulipa salio,” Wairimu alisema.
Familia imesema kuwa kwa sasa hawana namna ya kutoa mpendwa wao kutoka hospitalini na kuwa wanaisihi hospitali kuwasaidia kumzika mpendwa wao.