NA MWANDISHI WETU, DODOMA
WASTANI wa bei za mazao na bidhaa za chakula zimeshuka kwa asilimia 0.8 hadi 0.7 huku bei za vifaa vya ujenzi zikiendelea kupanda.
Naibu Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe amesema Dodoma Aprili 13, 2023 wakati akizungumzia mwenendo wa bei za bidhaa muhimu nchini kwa mwezi huu.
Kigahe amesema bei ya mahindi kwa Aprili ni kati ya Sh 800 na 1,650 kwa kilo ambapo imepanda kwa asilimia 1.5 ambayo ni sawa na ongezeko la Sh 25 kwa kilo, wakati bei ya chini imepungua kwa asilimia 5.9 sawa na punguzo la Sh 50 kwa kilo ikilinganishwa na bei ya Machi ambayo ilikuwa Sh 850 na Sh 1,625.
“Bei za chini zipo katika mikoa ya Ruvuma, Iringa na bei ya juu Pwani, Lindi na Mtwara,” amesema Kigahe.
Ameeleza kuwa unga wa mahindi mwezi huu ni kati ya Sh 1,200 na Sh 2,100 kwa kilo huku bei ya juu ikishuka kwa asilimia 20.0 sawa na kupungua kwa Sh 75 kwa kilo ikilinganishwa na Sh 1,400 na Sh 2,175 Machi mwaka huu.
Amesema bei ya mchele Aprili ni kati ya Sh 2,350 na Sh 3,500 kwa kilo ikilinganishwa na bei ya Sh 2,700 na Sh 3,600 kwa mwezi Machi.
Pia, maharagwe kwa mwezi huu ni kati ya Sh 2,175 na 3,800 kwa kilo ikilinganishwa na bei ya Machi ambayo ilikuwa kati ya Sh 2,988 na Sh 3,000 kwa kilo.
Aidha, bei ya viazi mviringo kwa Aprili ni kati ya Sh 900 na Sh 1,800 ikilinganishwa na bei ya mwezi Machi ambayo ilikuwa kati ya Sh 888 na Sh 2,000 kwa kilo 2,650 na 3,300 ikilinganishwa bei ya Machi ambayo ilikuwa kati ya Sh 2,700 na 3,125 kwa kilo.
Naibu Waziri amesema unga wa ngano kwa Aprili ni kati ya Sh 2,000 na 2,400 ikilinganishwa na bei ya mwezi Machi ambayo ilikuwa kati ya Sh 1,800 na 2,300 kwa kilo.
Amebainisha bei ya sukari kwa Aprili ni kati ya Sh 2,650 na 3,300 ikilinganishwa bei ya Machi ambayo ilikuwa kati ya Sh 2,700 na 3,125 kwa kilo.
Amesema bei ya mafuta ya kupikia ya alizeti kwa mwezi Aprili ni kati ya Sh. 4,000 na 8,500 ikilinganishwa na bei ya Machi iliyokuwa kati ya Sh.2,700 na Sh. 3,125 kwa kilo.
Akizungumzia mwenendo wa vifaa vya ujenzi, Naibu Waziri amesema bei ya saruji 42.5 kwa Aprili ni kati ya Sh.14,650 na Sh.24,500 kwa mfuko wa kilogramu 50 ikilinganishwa na bei ya Machi mwaka jana.
Amesema bei ya nondo mm 10 kwa Aprili ni kati ya Sh 16,000 na 23,500, bei ya juu imepanda kwa asilimia 6.8 sawa na Sh 1,500 ikilinganishwa na bei ya Machi mwaka jana ambayo ilikuwa Sh 22,000.
Aidha, amesema bei ya bati nyeupe geji 30 kwa Aprili ni kati ya Sh. 21,500 na Sh. 30,000 sawa na ongezeko la Sh. 2,500 ikilinganishwa bei ya Machi mwaka jana ambayo ilikuwa Sh. 27,500.