NA MWANDISHI WETU, RUVUMA
MIILI ya watu 13 waliofariki dunia kutokana na ajali ya gari aina ya Mitsubishi Fuso wilayani Songea wametambuliwa.
Kamanda wa Polisi mkoani Ruvuma, Marco Chillya amesema, ajali hiyo ilitokea jana majira ya saa 3 usiku katika eneo la daraja Njoka kijiji cha Namatuhi, barabara ya Ndongosi-Namatuhi wilayani Songea.
Amewataja waliofariki ni Happy Msemwa, Jaffery Juma Ngarimusi, Hidaya Salum, Bihesha Yahaya, Mustapha Ling’ole, Christopher Msuya, Mama Faraja na Deograsias Mapunda.
Kamanda Chillya amewataja marehemu wengine waliofahamika kwa jina moja moja ni Mwanaisha, Hamad ,Boniface na Simba ambao miili yao imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa Songea(HOMSO).
Amewataja waliojeruhiwa katika ajali hiyo ni Hamis Mbawala na Christopher Banda, ambao wamelazwa katika kituo cha afya Mpitimbi wakiendelea kupatiwa matibabu.
Amesema,ajali hiyo ilihusisha gari aina ya Mitsubishi Fuso yenye namba za usajili T-800BXB, iliyokuwa inaendeshwa na Thobias Njovu, ikitokea katika kijiji cha Ndongosi mnadani kuelekea kijiji cha Namatuhi, ambapo ilipinduka na kutumbukia mtoni na kusababisha vifo hivyo na majetruhi.