MIGORI, KENYA
WATU 10 wamepoteza maisha leo Jumamosi Aprili 8, 2023 katika Kaunti ya Migori nchini Kenya kutokana na ajali ya lori ambalo inaelezwa lilifeli breki na kuparamia kijiwe cha bodaboda.
Watu hao waliopoteza maisha inaelezwa ni vijana wa bodaboda waliokuwa wakisubiria wateja kwenye kijiwe chao.
Taarifa ya awali kupitia mtandao wa Tuko nchini Kenya imeeleza kuwa lori hilo la kubeba mchanga, lilipoteza mwelekeo na kugonga kundi la bodaboda ambao walikuwa pembezoni mwa barabara wakisubiri abiria.
Mashuhuda wa ajali hiyo wamesema muda mfupi eneo hilo lilitapakaa damu na miili ya watu ambapo juhudi za kuwaokoa waliopata majeraha zilikuwa zinaendelea.
“Miili yenye damu imesambaa katika eneo hilo na vyuma vinaonekana vimetapakaa damu,” ameeleza mmoja wa shuhuda ambaye hakutaka kutaja jina lake.
Umati mkubwa wa watu umemiminika eneo la tukio ili kuwanusuru majeruhi na kuwawahisha hospitalini kwa matibabu na wengine wakijaribu kuwatambua ndugu zao.
Shuhuda mwingine aliyezungumza na kituo cha runinga ya TV47, amesema breki za lori hilo inaonekana zilifeli na gari hilo kuingia katika kundi hilo la bodaboda ambao walikuwa wanasubiri abiria.
Ajali hiyo imetokea karibu na Shule ya Msingi ya Migori ambapo lilikuwa limejaa damu na miili kabla ya muda mfupi polisi kufika na kuwapeleka kuwahifadhi.
Kiongozi wa upinzani nchini humo, Raila Odinga ametoa pole kwa wafiwa ajali hiyo .