WELKOM, AFRIKA KUSINI
Rubani Rudolf Erasmus ambaye ni raia wa Afrika Kusini, amelazimika kuishusha ndege kutoka angani kwa dharura baada ya kubaini kuwepo nyoka aina ya cobra jirani na kiti chake.
Rubani huyo alikuwa akirusha ndege ndogo ya binafsi iliyokuwa na abiria wanne waliokuwa wakitoka Bloemfontein kwenda Pretoria Jumatatu wiki hii.
Shirikia la Habari la News24 limeeleza kuwa, Erasmus alishtuka akiwa angani, baada ya kuona nyoka mkubwa akitembea nyuma ya kiti chake.
Licha ya hofu kubwa aliyoipata, alilazimika kuishusha ndege kutoka angani kwa dharura katika mji wa Welkom uliopo katikati na eneo walilokuwa wakielekea.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Afrika Kusini (SACAA), Poppy Khoza amempongeza rubani huyo kutokana na ujasiri wake na uamuzi aliouchukua kunusuru maisha ya abiria aliokuwa nao.
“Ninakupongeza Rudolf kwa hatua uliyoichukua na kudhibiti hatari iliyojitokeza angani pia kuwa umakini licha ya ukweli kwamba ingekuwa ajali kubwa,” amesema.
“Umekuwa mtulivu licha ya kukutana na tukio la hatari akiwa angani na kumudu kuishusha ndege kwa hali ya utulivu bila kusababisha madhara kwa abiria yeyote. Umeonesha uhodari na umekuwa balozi mzuri katika masuala ya anga duniani,” amesema mkurugenzi huyo.
Rubani huyo ameeleza kwamba awali aliposikia kitu kikitembea alidhani ilikuwa ni chupa yake ya maji lakini baadaye alibaini kilikuwa ni kitu tofauti. Hivyo hakuweza hata kujitikisa.
Aina hiyo ya nyoka wanaoitwa Cape Cobra mara nyingi wanapatikana Kusini Magharibi mwa Afrika na wana sumu kali pia wakikuuma unahitaji matibabu ya haraka bila kuchelewa.