NA MWANDISHI WETU, TANGA
SERIKALI mkoani Tanga, imesema itaendelea kutoa ushirikiano kwa taasisi na mashirika binafsi kwa kuweka mazingira rafiki, ili yaweze kufanya shughuli za maendeleo kwa ufanisi .
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Waziri Kindamba Aprili 5, 2023 wakati alipotembelewa na viongozi wa taasisi ya Islamic Help ofisini kwake, ambapo wametoa taarifa mbalimbali za miradi ya maendeleo wanayoitekeleza kwenye wilaya mbalimbali mkoani hapa.
Amesema kuwa viongozi wa mkoa huo wapo tayari kutoa ushirikiano kwa taasisi mbalimbali, ili kuunga mkono jitihada za serikali za kuwafikishia maendeleo wananchi.
“Lengo la serikali ni kupeleka huduma bora kwa wananchi, hivyo yanapokuwepo mashirika binafsi kama Islamic Help yanasaidia kumaliza changamoto za kimaendeleo, ikiwemo kusogeza huduma karibu na jamii,”alisema RC Kindamba.
Meneja Rasilimali watu wa Islamic Help, Tittee Zubeir amesema kuwa katika kipindi cha miaka miwili, shirika hilo limefanya uwekezaji wa miradi mbalimbali yenye thamani ya Sh Bil 11.5.