NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
TUME ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) imeiomba Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia kumualika Rais wa Tanzania Samia Suluh Hassan kushiriki kwenye Kongamano la Kitaifa la maonesho ya Sayansi na Ubunifu linalotarajiwa kufanyika Juni 14-16 mwaka huu.
Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH Dk. Amos Nungu ameyasema hayo Aprili 4, 2023 jijini Dar es Salaam wakati wa kutambulisha uwepo wa kokangamano hilo litakalokuwa na kauli mbiu ‘sayansi na ubunifu kwa maendeleo endelevu’ litakalofanyika katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere Dar es Salaam
Dk. Nungu alisema, Kongamano hilo ni mkakati wa Tume katika kutekeleza majukumu yake ya msingi kwa kuhabarisha umma wa Tanzania na Dunia kwa ujumla juu ya kazi zake na ushirikiano uliopo kati ya watafiti wa ndani na nje ya nchi.
“Lengo kubwa la kongamano hilo ni kuwawezesha watafiti, wabunifu,wanasayansi na watunga Sera kukutana pamoja ili kujadili,kubadilishana mawazo na kupeana taarifa mbalimbali juu ya masuala ya Teknolojia na ubunifu nchini”. alisema Dk.Nungu.
Ameongeza kuwa, katika malengo hayo wamenyumbulisha mambo mbalimbali ikiwemo kuishauri serikali na vyombo vyake kupitia matokeo ya kitafiti zinazofanywa kwa ajili ya maendeleo ya nchi lakini pia watafiti na wabunifu kupata fursa ya kusikiliza kutoka kwa wafanya maamuzi na watunga sera kuhusu mipango ambayo watafiti na wavumbuzi waweze kuifata miongozo hiyo.
Dk. Nungu amesema katika kongamano hilo wabunifu na wavumbuzi watapata fursa ya kusikiliza kutoka katika serikari na wizara zake mbalimbali zinamipango ipi ambayo wao wanaweza kuendana nayo na endapo changamoto yoyote itatokea watafuata miongozo itakayo kuwepo.
Dk. Nungu ameeleza kuwa bunifu zipo nyingi lakini wabunifu wanatakiwa kuwa na bunifu zinazoangalia mbele zaidi na wenye kuleta maendeleo Tanzania.
“Watafiti, wabunifu na wanasayansi mbali mbali wafanya maamuzi ili kujadili na kutoa mawazo mbalimbali kuhusu wizara ya Sayansi na Teknolojia.
Sambamba na hayo ameeleza kupitia kongamano hilo wataweza kuwatambua watafiti waliopokea tuzo baada ya Waziri wa Sayansi na Teknolojia alipozindua rasmi tuzo ya utafiti mchakato utakapokamilika.
Aidha Dk. Nungu ameongeza kuwa COSTECH itaendelea kuwaunga mkono vijana wabunifu ili waweze kunufaika na bunifu mbalimbali wanazozifanya.