NA MWANDISHI WETU, MWANZA
MKAZI wa Kitongoji cha Kasuzu Kata ya Namagondo Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza, Anselumu Sebuka (42) amejaribu kujiua kwa kujikata uume wake.
Taarifa ya Jeshi la Polisi mkoani Mwanza kwa vyombo vya habari inasema tukio hilo limetokea Aprili Mosi, 2023 Saa 2:00 usiku ambapo Sebuka alikata uume wake kwa kutumia kisu chenye ncha kali na kuuacha ukining’inia.
“Alikutwa ndani ya chumba chake akiwa amejaribu kujiua kwa kukata uume wake kwa kutumia kisu chenye ncha kali, inadaiwa alikuwa anatuhumiwa na ndugu zake kuiba mali mbalimbali za familia yake na za jamii inayomzunguka na kwenda kuziuza,”inasema taarifa hiyo iliyosainiwa na Kamanda wa Polisi mkoani humo, Wilbroad Mutafungwa
Taarifa hiyo inasema pamoja na kutuhumiwa kujihusisha na tabia ya wizi, Sebuka alitengwa na familia yake kutokana na ulevi uliokithiri ndipo alipoamua kujaribu kutoa uhai wake.
“Chanzo cha tukio hilo ni ugomvi wa kifamilia uliosababisha kupata msongo wa mawazo. Sebuka alipelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Ukerewe kwa ajili ya matibabu na hali yake inaendelea vizuri,”
Jeshi hilo la Polisi limewataka wananchi kufuata njia sahihi za kutatua matatizo yao ikiwemo kuwaona wataalamu wa afya ya akili ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na msongo wa mawazo na kukosa uvumilivu wa migogoro mbalimbali katika jamii.