NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Maliasili na Utalii Mohamed Mchengerwa anatarajiwa kuzindua kitabu cha Hoja Kinzani kuhusiana na masuala ya uhifadhi wa maliasili nchini kilichoandaliwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Ndaki ya Sayansi ya Jamii.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Aprili 3, 2023 Rasi wa Ndaki hiyo ya Sayansi ya Jamii, Profesa Christine Noe amesema kitabu hicho ambacho ni hitimisho la mradi wa utafiti ulioitwa ‘Ushirikiano mpya katika uhifadhi, maendeleo ya kiikolojia na jamii’ kinatarajiwa kuzinduliwa kesho Aprili 4, 2023.
Prof. Noe amesema kwa takriban miongo mitatu sasa kumekuwa na ongezeko kubwa la ushirikishwaji wa jamii katika kuhifadhi maliasili huku wadau mbalimbali wakiungana na Serikali ya Tanzania katika kubadili mtazamo na mwenendo wa uhifadhi.
“Hivyo lengo kuu la kitabu hiki lilikuwa ni kuangalia kama ongezeko ilo la ushirikiano katika shughuli za kuhifadhi wa maliasili umeongeza ufanisi au la hasa katika kuimarisha uhifadhi wenyewe na maendeleo ya jamii.
“Hata hivyo ni dhahiri kwamba ongezeko kubwa la wadau na washiriki katika uhifadhi wa maliasili umelenga kwenye kutafuta maendeleo endelevu katika uhifadhi na kuleta maendeleo kwa jamii zinazozunguka maeneo yaliyohifadhiwa,” amesema Prof. Noe
Prof Noe amesema katika kitabu hicho ambacho kinazinduliwa leo kinaonyesha ni namna gani juhudi za ushirikiano wa wadau wa hifadhi zimekuwa na matokeo tofauti tofauti.
“Kitabu hiki kimechakata taarifa za kila sekta kuangalia kama ushirikishwaji wa jamii na ongezeko la wadau mbalimbali kwenye uhifadhi wa maliasili kumeleta matokeo chanya kwa mazingira na maisha ya watu na je sehemu zenye ushirikiano wa wadau wengi kunatofauti gani na sehemu zenye ushirikiano wa wadau wachache,” amesema Prof. Noe
Aidha Prof Noe amesema kitabu hicho kimehitimisha kwa kueleza kuwa bado uhifadhi haujaweza kuwa tegemeo katika kuleta maendeleo kwa jamii za wakulima na kwamba tofauti ipo kidogo kwa jamii zinazopakana na hifadhi za misitu kwani sera za misitu zimetoa fursa za uvunaji unaowezesha jamii kuongeza kipato.