NA MWANDISHI WETU, MANYARA
MKAZI wa Kijiji cha Kidoka wilayani Chemba, Mkoa wa Dodoma, Tano Shabani (31) amepoteza maisha baada ya kusombwa na maji wakati akiendesha trekta akiwa na msaidizi wake ambaye alinusurika kifo baada ya kukwama kwenye mizizi ya miti Kijiji cha Mwanya Wilayani Kiteto.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Manyara, RPC George Katabazi akizungumza Machi 31, 2023 amesema tukio hilo limetokana na mvua kubwa iliyonyesha na kusababisha mafuriko Machi 30, 2023.Hivyo wakati wanavuka wakiwa na trekta lao kwenye korongo la Kijiji cha Mwanya, Kiteto hawakujua kuwa maji hayo yalikuwa mengi kuwa wasingeweza kupita.
“Hili trekta na dereva wake walikuwa wakijaribu kuvuka kwenye mkondo wa maji ambayo yalikuwa yakikatisha barabara bila kuchukua tahadhari kisha kusombwa na maji na baada ya kusombwa dereva Tano Shambani (31) yeye alifariki dunia,” amesema.
Kwa upande wa msaidizi wake, John Juma (23) wote wakazi wa Kidoka wilayani Chemba mkoani Dodoma alinusurika kwa sababu baada ya kusombwa na maji alikwama kwenye mizizi ya miti kisha kupanda juu ya mti huo.
Tukio jingine ni la watu wawili walionusurika kifo kwa ajali ya lori kampuni ya Pepsi lililokuwa limebeba vinywaji baridi aina ya Pepsi mjini Kibaya ambalo lilifeli breki na kurudi nyuma na kutumbukia korongoni.
“Hilo lori ambalo Kampuni ya Pepsi lilikuwa na vinywaji baridi aina ya Pepsi likipanda mwinuko ambapo mfumo wa breki ulifeli likaanza kurudi nyuma na kudumbukia korongoni ambapo gari hilo limehatibika vibaya baada ya kuanguka, ” amesema.
Amesema dereva wa gari hilo hajapata madhara makubwa pamoja na msaidizi wake akidai uharibifu mkubwa ni ule wa gari hilo pamoja na vinywaji vilivyokuwa vimepakiwa vya chupa kuvunjika.
Kamanda Katabazi ametoa wito kwa madereva kuchukua tahadhari wanapoendesha vyombo vya moto akisema kila kukicha madhara yanaendelea kujitokeza kwa ajali hizo na kama madereva wangeweza kuchukua tahadhari wangenusuru maisha ya watu na kuepuka hasara.