NA MWANDISHI WETU, RUANGWA
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezindua jengo la wagonjwa wa dharura kwenye hospitali ya wilaya ya Ruangwa ambalo limegharimu sh. milioni 390.
Akizungumza na wakazi wa Ruangwa waliofika kushuhudia uzinduzi huo leo Ijumaa, Machi 31, 2023, Waziri Mkuu amesema ameridhishwa na ujenzi huo na hasa kwa vile amekuta kuna vifaa vya kisasa.
“Yote haya ni matunda ya kazi nzuri inayofanywa na Rais wetu, Mheshimiwa Dk Samia Suluhu Hassan na yamesaidia kuifanya wilaya yetu iwe miongoni mwa wilaya zinazoenda kwa kasi,” amesema.
Waziri Mkuu amesema hospitali hiyo imejengwa kwenye eneo lenye ukubwa wa ekari 100 ambalo kazi ya kujenga uzio ni kubwa kwa hiyo akawataka wakazi hao wawe walinzi wa miundombinu na vifaa tiba vilivyonunuliwa ili waendelee kupata huduma bora na za uhakika.
“Eneo hili lina ekari 100. Ninaomba sana sisi tuwe walinzi wa vifaa hivi vilivyopo hapa ndani na kamwe tusishiriki mpango wowote wa kurudisha maendeleoa nyuma,” amesisitiza.
Naye, Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel amesema Serikali ya awamu ya sita ndani ya mwaka mmoja imetoa sh. bilioni 51.4 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali za Taifa na Kanda.
“Kwa ajili ya Hospitali za Mikoa nchi nzima, Rais wetu ametoa sh. bilioni 54.2 na kwenye eneo la vifaa, ndani ya mwaka huu mmoja ametoa shilingi bilioni 290.9,” amesema.
Naye, Naibu Waziri wa Nchi (OR-TAMISEMI), Dk. Festo Dugange amesema jengo hilo lililozinduliwa ni miongoni mwa majengo 80 yaliyojengwa nchini kwa kutumia fedha za UVIKO-19. Katika mkoa wa Lindi, majengo kama hayo yamejengwa pia katika wilaya za Liwale na Kilwa.
Amesema katika awamu ya kwanza, wilaya hiyo ilipokea sh. bilioni 2.9 ambazo majengo yake yamekamilika na sasa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ameleta sh. milioni 800 za kujenga wodi za kisasa ambazo zitakuwa na vifaa vya kisasa pia.
Mapema, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Dk.Salvio Wikesi amesema mradi huo unatarajiwa kuwa na majengo 22 ambayo hadi kukamilika kwake yanatarajiwa kugharimu sh. bilioni 7.5.
“Hospitali inaendelea na ujenzi wa majengo matano ya awamu ya tatu ambayo ni jengo la huduma za dharura, jengo la upasuaji, jengo la kuhifadhia maiti, jengo la wodi ya upasuaji wanaume na wodi ya upasuaji wanawake.”
“Hadi sasa, mradi umegharimu kiasi cha sh.milioni 390.72 ikiwa ni ongezeko la vifaa na kiasi cha sh.milioni 90.72 ambazo zimetumika kuimarisha eneo la hospitali kwa kuwa lilikuwa na maji mengi chini ya ardhi na hivyo maandalizi ya ujenzi kuanzia hatua ya msingi hadi jamvi yalihitaji uimarishaji msingi wa jengo.”
Ameeleza kuwa, pamoja na ukamilishaji wa jengo hilo, Serikali pia ilitoa vifaa tiba vya kisasa na Wizara ya Afya ikapeleka mashine ya x-ray, mashine ya kutakasia vifaa kabla ya kufanya upasuaji na mashine ya kumfanyia uangalizi mgonjwa wakati wa upasuaji.