NA MWANDISHI MAALUM, LINDI
JUMLA ya vijiji 55 mkoani hapa vinatarajia kunufaika na mradi wa maji utakaogharimu sh.Bil 119/-.
Kati ya vijiji hivyo 34 ni vya wilaya ya Ruangwa na 21 ni vya wilaya ya Nachingwea.
Hayo yameelezwa leo Machi 31, 2023 na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akizungumza na maelfu ya wakazi wa Ruangwa waliohudhuria hafla ya kutambulisha mafanikio ya miaka miwili ya Serikali ya awamu ya sita iliyofanyika kwenye ghala la Lipande, wilayani hapa.
Waziri Mkuu amesema kuwa, mradi huo ambao utaanzia Nyangao kwenda Nanganga hadi Ruangwa kisha utaenda Chiola hadi Nachingwea.
Ameeleza kuwa, Mkandarasi ameshapatikana na mkataba umeshasainiwa. Kwa hiyo mradi utaanza wakati wowote.
“Dhamira ya Rais wetu Dk Samia Suluhu Hassan ni kuongeza uwezo wa upatikanaji wa maji kwenye miji yetu na vijiji vinavyozunguka miji hiyo.”amefafanua Waziri Mkuu
Waziri Mkuu ambaye pia ni Mbunge wa Ruangwa, ametumia fursa hiyo kuelezea mafanikio yaliyopatikana kwenye sekta za elimu, afya, maji, barabara, madini na michezo.
Kuhusu mafanikio ya elimu kwenye wilaya hiyo, Waziri Mkuu amesema miundombinu imeboreshwa kwa kujenga shule mpya za sekondari na za msingi, ufundishaji umeimarika na ufaulu kuongezeka na kufikia asilimia 98.
Amesema wilayani humo kuna baadhi ya kata ambazo zina shule za sekondari mbili ambapo kata ya Likunja ina sekondari za Likunja na Kitandi.
“Kata nyingine ni Narungombe kuna ambako kuna sekondari za Liugulu na Narungombe ambapo Liugulu tumeamua iwe ni maalum kwa wasichana na Narungombe iwe maalumu kwa wavulana. “
Waziri Mkuu amewapongeza walimu na wazazi kwa kuweza kudhibiti utoro wa wanafunzi na aliwapongeza wazazi kwa kusimamia nidhamu ya watoto wao na kufuatilia masomo yao.
“Tukifanya haya, tutaongeza nguvu ya walimu na azma yetu ya kutoka asilimia 98 kwenda 100 itafikiwa,” amesema.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Abuu Jumaa ambaye alikuwepo kwenye hafla hiyo aliwataka wazazi wachukue tahadhari kwa watoto wao katika kipindi hiki ambacho kinakabiliwa na mmomonyoko wa maadili.
“Dunia imeharibika, sasa hivi kuna jambo la ushoga linaendelea. Nawaomba wazazi na wananchi wa Ruangwa tukae na watoto wetu na tulisemee jambo hili. Pia UKIMWI bado upo, tatizo la dawa za kulevya lipo, yote haya lazima tuyasemee kwa vijana wetu”
Wakati huo huo, Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel amekabidhi nyaraka za ununuzi wa dawa za mkoa mzima zenye thamani ya sh. bilioni 2 /-kwa Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Tellack ili aweze kuzifuatilia kwa makini kwa kila wilaya.
Dk Mollel amesema mgao wa mkoa mzima ulikuwa sh. bilioni 6/- lakini hadi sasa mkoa umeshatumia sh. bilioni 4/-.
Naye, Naibu Waziri wa Nchi ofisi ya Rais( OR TAMISEMI), Dk Festo Dugange amesema Serikali inatambua kuwa Halmashauri hiyo ina upungufu wa magari ya wagonjwa na imeshalifanyia kazi suala hilo.
“Serikali imenunua magari matatu kwa ajili ya Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa ambapo mawili kati ya hayo ni magari ya kubeba wagonjwa na gari moja ni la kusafirisha chanjo. Pia watumishi wa afya tumewaleta, wapo 67 na walimu walioletwa hapa wapo 91,” amehitimisha