NA MWANDISHI WETU, HANDENI
WATU watatu wa familia moja wamefariki dunia kwa kuteketea na moto, baada ya lori lililobeba gesi kupinduka na kuwaka moto uliosambaa kwenye nyumba zao katika Kijiji cha Kwamachalima wilayani Handeni mkoani Tanga.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa Polisi mkoani Tanga, Henry Mwaibambe amesema kuwa ajali hiyo imetokea leo Ijumaa Machi 31, 2023 majira ya saa 11 alfajiri ambapo dereva wa lori alieleza kuwa chanzo ni kupasuka tairi ya mbele upande wa kushoto.
Amesema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ili kubaini kama ni kweli chanzo ni tayari, kwani mashaka ni mengi kutokana na tukio hilo.
“Hadi sasa tuna majeruhi tisa wanawake watano na wanaume wanne wapo kituo cha afya Kwabuku na hali zao sio mbaya, ila waliopeteza maisha ni watatu,” amesema Kamanda Mwaibambe.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Albert Msando amesema Serikali itahakikisha usalama wa wananchi wa eneo hilo wakati gari lenye gesi likiwa bado halijaondolewa.
Amesema ukiacha vifo na majeruhi madhara mengine yaliopatikana ni kuharibika miundombinu ya umeme yenye thamani ya zaidi ya Sh.Milioni 250.