NA MWANDISHI WETU, SINGIDA
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Singida imemhukumu kifungo cha maisha mkazi wa Mtaa wa Majengo, Fabiano Dubabe kwa kosa la kuwabaka na kuwalawiti watoto wake watatu.
Dubabe, aliyekuwa akijishughulisha na kazi ya ulinzi anatuhumiwa kutenda makosa hayo kati ya mwaka 2018 na 2022 kwa nyakati tofauti.
Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Robert Oguda amesema Mahakama imeridhishwa bila kuacha shaka kuwa, mtuhumiwa alitenda makosa hayo kinyume na sheria ya adhabu.
Amesema ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka umethibitisha bila kuacha shaka kwamba, mshtakiwa ana hatia kama alivyoshitakiwa.
“Mshtakiwa, Mahakama hii inakutia hatiani kwa makosa mawili ya kubaka watoto wako wawili wa kike kwa nyakati tofauti na kila kosa utatumikia jela miaka 30.
“Lakini unatiwa hatiani kwa makosa matatu ya kumwingilia kinyume na maumbile mtoto wako wa kiume, kila kosa utatumikia jela maisha yako yote,” amesema Hakimu Oguda.
Mwanasheria wa Serikali na Mwendesha Mashtaka, Nuru Chiwalo amesema mbele ya Mahakama hiyo kuwa mshtakiwa alitenda makosa hayo kati ya mwaka 2018 na 2022.
Chiwalo amesema jumla ya mashahidi 18, akiwamo mke wa mshtakiwa kwa nyakati tofauti walitoa ushahidi dhidi ya Fabiano.
Wakati akijitetea, mshtakiwa aliomba kupunguziwa adhabu kutokana na hatia aliyokutwa nayo kwa kuwa ana familia inayomtegemea.