NA FARIDA RAMADHANI, DODOMA
NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Lawrence Mafuru amesema kuwa Serikali inafanya majadiliano ya kimkakati na Benki ya Dunia (WB) namna ya kuiwezesha sekta binafsi kushiriki katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kupitia mpango wa ushirikiano kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi, yaani PPP.
Ameeleza hayo jijini Dodoma baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Benki ya Dunia ulioongozwa na Mkurugenzi Mkazi wa Benki hiyo Nathan Belete, ambapo walijadili namna bora ya utekelezaji wa sheria ya PPP pamoja na uboreshaji wa mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara nchini.
Amesema majadiliano hayo ni utekelezaji wa msisitizo na maelekezo yanayotolewa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kuwa sasa ni wakati wa Sekta Binafsi kushirikiana na Serikali kwa ajili ya kuleta maendeleo ya kiuchumi.
Mafuru amesema Rais Dk Samia Suluhu Hassan amesisitiza kila wakati kuwa pale ambapo Sekta Binafsi inaweza kufanya jambo fulani basi hakuna haja ya kutumia fedha za Serikali, lakini changamoto ilikuwa ni namna na mfumo ambao unaweza kusaidia miradi kufanyika kwa njia ya PPP.
“Wenzetu wa Benki ya Dunia wamekua mstari wa mbele katika kutoa fedha sio tu katika miradi ya kijamii, lakini sasa wanajielekeza zaidi kutoa fedha na misaada ya kitaalam kuhakikisha kwamba eneo hili la PPP sambamba na uboreshaji wa mazingira ya uwekezaji na biashara nchini yanafanikiwa”, amesema Mafuru.
Amesema kwa sasa Serikali imeanza majadiliano ya awamu ya pili na Benki ya Dunia kuhusu msaada ambao umejielekeza kwenye sekta za miundombinu na sekta zitakazoboresha mazingira ya kufanya biashara nchini.
Aidha, amebainisha kuwa Sheria ya Ushirikiano kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP) inafanyiwa marekebisho ili iweze kuwa shindani, ambayo itaweza kuvutia mitaji ya Sekta Binafsi na hatimaye kiwezesha sekta hiyo kushirikiana na Serikali katika kutekeleza miradi.
Amesema hatua hiyo itaweza kuipunguzia Serikali mzigo wa kibajeti ili fedha ambazo zilipangwa kutumika kwenye miradi ambayo inaweza kufanywa na Sekta Binafsi zielekezwe kwenye sekta za kijamii ambazo haziwezi kuvutia Sekta Binafsi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Belete amesema benki hiyo imeamua kujadiliana na Tanzania kuhusu namna bora ya utekelezaji wa miradi kwa njia Sekta ya Umma na Binafsi (PPP) kwa kuwa ni miongoni mwa vipaumbele vya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Ameeleza kuwa majadiliano na Serikali yalikuwa mazuri na anaamini kwamba makubaliano yao yataleta mabaliko katika mfumo wa utekelezaji wa PPP nchini na kuchochea maendeleo ya nchi.
Belete ameahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania kwa karibu katika kutekeleza matarajio ya maendeleo.
.