NA BENNY MWAIPAJA, DAR ES SALAAM
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amewahimiza wawekezaji kutoka Austria na Ujerumani, kuharakisha mchakato wa kuwekeza katika sekta ya ujenzi wa makazi ya kisasa na ya gharama nafuu ili kutatua changamoto ya makazi hususan kwenye taasisi za umma hapa nchini.
Dk.Nchemba ametoa wito huo alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa wawekezaji kutoka Austria na ujerumani, ukiongozwa na Waziri Mkuu Mstaafu wa 10 wa Austria, Dk Alfred Gusenbauer, jijini Dar es Salaam.
Wawekezaji hao wameonesha nia ya kuwekeza kwenye ujenzi wa nyumba zenye gharama nafuu zinazotumia teknolojia ya kisasa na rafiki kwa mazingira, sekta ya misitu, kilimo na kuwezesha upatikanaji wa mitambo inayotumika kupakia na kupakua mizigo bandarini.
Dk. Nchemba amesema kuwa kuna uhaba mkubwa wa makazi katika sekta za afya, elimu na makazi binafsi hivyo aliwahimiza wawekezaji hao kukamilisha majadiliano na wataalam wa sekta husika ili kama kutakuwa na maridhiano ya gharama nafuu kwa kuzingatia ubora wa makazi hayo, basi mradi huo uanze kutekelezwa.
Amesema kuwa hivi sasa Serikali iko katika mchakato wa kuandaa Bajeti mpya ya mwaka wa fedha 2023/2024 hivyo kama mradi huo utaanza kutekelezwa kwa kutumia mikakati tofauti ikiwemo kuishirikisha sekta binafsi, serikali itaelekeza fedha zilizopangwa kutumika kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu hiyo kwenye sekta nyingine za huduma za jamii.
Kwa upande wai, Waziri Mkuu Mstaafu wa kumi wa Austria, na Kiongozi wa Ujumbe wa wawekezaji hao, Dk Gusembauer, walisema kuwa wamefurahishwa na mazingira tulivu ya uwekezaji yaliyopo nchini na kwamba wanatarajia kuwekeza kwenye sekta muhimu.
Amesema wanatarajia kuwekeza kwenye ujenzi wa makazi nafuu ya nyumba za walimu, ujenzi wa hospitali hospitali na nyumba za wahudumu wa afya, ujenzi wa makazi biafsi ya watu pamoja na hifadhi ya misitu na kueleza kuwa mkutano kati yao na Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba ulikuwa wenye manufaa makubwa.
Mkutano huo ulimshirikisha pia Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk.Angelina Mabura, Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu, Kamishna wa Idara ya Usimamizi wa Madeni Wizara ya Fedha na Mipango, Japhet Justine na Viongozi wengine kutoka Serikalini.