NA MWANDISHI WETU, TABORA
WATU 13 akiwemo Mtemi wa Sungusungu na Mwenyekiti wa kijiji cha Isakamaliwa mkoani Tabora wamefikishwa Mahakamani wakishtakiwa kwa mauaji ya wafugaji watatu wa Kata ya Isakamaliwa, wilayani Igunga.
Mbele ya Hakimu wa Wilaya ya Igunga, Lyidia Ilunda Mwendesha Mashtaka wa Polisi wilayani humo, Ellymajid Kweyamba amemtaja mshtakiwa wa kwanza, Jijadi Katambi (43) ambaye ni Mtemi wa jeshi la Jadi la Sungu-sungu kata ya Isakamaliwa.
Washtakiwa wengine ni Mwenyekiti wa serikali ya Kijiji cha isakamaliwa, Shija Mboje (48), Michael Masanja (36), Mwalimu wa shule ya msingi Isakamaliwa, Kulala Shigela (38) Masunga Kulwa (39) na Nkwabi Mipawa (58), Maleba Machenge (37), Ngoga Ifegelo (50), Ndulu Manyenye (32), Shakali Ifegelo (30), Magembe Mwandu (25), Mahona Jilala (35) na Bakari Hamis (45) wote wakazi wa kata ya Isakamaliwa.
Majid amesema leo Jumatatu Machi, 27,2023 kuwa katika shtaka la kwanza linalowakabili washitakiwa hao ni kwamba Mei 12, 2022 mchana katika Kijiji cha Isakamaliwa na kata ya Isakamaliwa wakiwa na nia ovu walimuua Darushi Bukwere (26) mkazi wa kata ya Isakamaliwa.
Katika shtaka la pili amesema tarehe hiyo washtakiwa hao wakiwa na nia ovu walimuua Gwisu Manyenye (30) mkazi wa Kijiji cha Isakamaliwa huku akisema shitaka la tatu linalowakabili washitakiwa hao ni siku hiyo hiyo kumuua Jacob Tungu (32)mkazi wa kata hiyo.
Majid ameiambia mahakama kuwa washitakiwa wote, wametenda makosa hayo kinyume na kifungu cha 196 kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2019.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo matatu, washtakiwa wote hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo ambapo kesi hiyo imeahirishwa hadi Machi 30, 2023 itakapotajwa tena na washtakiwa wote wamepelekwa mahabusu.