NA MWANDISHI WETU, NEWALA
MAHAKAMA ya Wilaya ya Newala mkoani Mtwara imemhukumu kifungo cha miaka 30 Jela, Selemani Mtipa maarufu kama Sele Mkazi wa Wilaya hiyo kutokana na kumtia hatiani baada ya kukiri kutenda kosa la kuruhusu kuingiliwa kinyume na maumbile na wanaume mbalimbali.
Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mwandamizi/Mfawidhi Innocent Sotter mbele ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Salehe Mganga baada ya Mshtakiwa kukiri kutenda kosa hilo, kwa nyakati tofauti baada ya kuruhusu wanaume mbalimbali kumuingilia kinyume na maumbile.
Mshtakiwa huyo ameadhibiwa kwa kosa la kuruhusu kuingiliwa kinyume na maumbile kinyume na kifungu 154(1)(c) cha kanuni ya adhabu sura na 16 iliyofanyiwa marejeo ya mwaka 2022.
Baada ya mshtakiwa kutiwa hatiani upande wa mashtaka haukuwa na kumbukumbu ya makosa ya awali lakini waliomba Mahakama imuadhibu kwa mujibu wa kifungu cha 154 cha kanuni ya adhabu ili iwe fundisho kwake na onyo kwa jamii nzima kwa kuwa vitendo hivyo vimekuwa vikiongezeka na kusababisha mmomonyoko wa maadili.
Aidha mshtakiwa alipewa nafasi ya kujitetea ambapo aliiomba Mahakama impunguzie adhabu kwa kuwa atajirekebisha.
Washitakiwa wengine wawili walikana kutenda makosa kama hayo na kurudishwa rumande baada ya kukosa wadhamini na shauri lao litaendelea Machi 27, 2023 kwa uchambuzi wa hoja za awali.