NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
MAOFISA wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela), wametoa mafunzo kwa wanafunzi 80 wa chuo cha Uhasibu Tanzania (TIA), ikiwa ni mwendelezo wa jitihada za Taasisi kuhakikisha kuwa elimu kuhusu urasimishaji wa Biashara inawafikia wadau mbalimbali nchini.
Mafunzo hayo yametolewa chuoni hapo Machi 25 , 2023 Kurasini, jijini Dar es Salaam kwa wanafunzi wanaosoma Fani ya Usimamizi wa Biashara (Business Administration).
Wanafunzi hao wamewapatiwa elimu kuhusu taratibu za usajili wa kampuni, Majina ya Biashara, Alama za Biashara na Huduma, utoaji wa Hataza pamoja utoaji wa Leseni za Biashara Kundi “A” na Viwanda.
Pia wameelekezwa kwa vitendo jinsi ya kutuma maombi mbalimbali kupitia Mfumo wa Usajili kwa njia ya Mtandao (ORS).
Ofisa Sheria wa Brela, Lupakisyo Mwambinga akiwasilisha mada kuhusu utaratibu wa Usajili wa Kampuni na Majina ya Biashara ameeleza kuwa urasimishaji wa biashara unawezesha kupata fursa mbalimbali na kupanua wigo wa kibiashara.
Kwa upande wa Msaidizi wa Usajili wa Brela, Abdulkarim Nzori ameeleza jinsi Miliki Ubunifu inavyoweza kuwanufaisha wabunifu mbalimbali, kwakuwa ubunifu wowote unaanza na binadamu, hivyo ni vyema wakasajili bunifu zao ili kuwanufaisha wao na Taifa kwa ujumla.