Thomas Tuchel kumng’oa kocha Chelsea na wachezaji wawili
Mjerumani Thomas Tuchel (49) anafikiria kwenda kumng’oa kocha msaidizi wa Chelsea, Muingereza Anthony Barry (36), ili awe msaidizi wake kwenye kibarua cha kuinoa Bayern Munich iliyompa kazi jana akichukua nafasi ya Nagelsmann. Bayern walifanya haraka kumteua Tuchel kutokana na hofu kwamba huenda akachukuliwa na Real Madrid au Tottenham.
Tuchel pia atajaribu kumsajili mlinda mlango wa Senegal, Edouard Mendy (31) na kiungo wa kati wa Croatia, Mateo Kovacic (28) kutoka klabu yake ya zamani ya Chelsea ili kukiimarisha kikosi cha Bayern.
Julian Nagelsmann kwenye rada za Tottenham Hotspur
Tottenham Hotspur wamemuweka kwenye rada zao kocha Julian Nagelsmann (35) aliyefukuzwa kazi Bayern Munich jana Ijumaa, Machi 24, 2023 kama mbadala wa Muitaliano Antonio Conte (53) aliyekalia kuti kavu klabuni hapo.
Lakini Nagelsmann ndoto zake ni kuifundisha Real Madrid ambayo meneja wake Muitaliano Carlo Ancelotti (63) akiwa hana uhakika na mistakabali wake.
Barca wamsaka Gundogan
Barcelona wameonyesha nia ya kumsajili kiungo wa kati wa Manchester City na Ujerumani, Ilkay Gundogan (32). Mawakala wa mchezaji huo wamesema upo uwezekano wa mchezaji huyo kutua Hispania kama dau litaeleweka.
Arsenal wafikiria kumalizana na Pepe
Arsenal wanataka kumuuza mchezaji wao aliyeweka rekodi ya uhamisho Nicolas Pepe (27), ambaye kwa sasa anakipiga kwa mkopo kwenye klabu ya Nice msimu huu. Lakini itawalazimu Arsenal kumlipa mchezaji huyo wa kimataifa wa Ivory Coast ili kuondoka.
PSV wamuweka sokoni Sangare
PSV Eindhoven wako tayari kumuuza kiungo wao wa kati raia wa Ivory Coast, Ibrahim Sangare (25). Tayari Arsenal, Chelsea, Liverpool na Tottenham zimeonyesha nia ya kumsajili.
Chelsea wakubali kuandaa mechi ya Ukraine.
Mmiliki wa Chelsea, Todd Boehly amekubali kwa muda kuandaa mechi ya nyota wote ya kuchangisha fedha katika uwanja wa Stamford Bridge mwezi Agosti kwa ushirikiano na shirika la kutoa misaada la Football for Ukraine. (Evening Standard)