NA MWAMDISHI WETU, MANYARA
JESHI la Polisi Kiteto Mkoani Manyara, linawashikilia wanawake wawili, eneo la Njutaa Kijiji cha Kimana, Kata ya Partimbo Kiteto wilayani Kiteto mkoani Manyara, kwa tuhuma za kukutwa na wanyama kwenye makazi yao.
Jeshi hilo limesema limewakamaata wanawake hao wakiwa na nyama ya Mbawala (Pongo) na mnyama hai aina ya Digidigi.
Akizungumza na vyombo vya habari leo Machi 22, 2023, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Manyara, George Katabazi amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Veronica Paulo Mnubi (24) na Witness Paulo Mnubi (20) wote wakazi wa eneo la Njutaa Kijiji cha Kimana.
Nyara hizi za Serikali ni nyama pori aina ya Mbawala (Pongo) ambayo imekadiriwa kuwa na thamani ya Sh1.4 mil, lakini pia walikutwa na mnyama pori hai aina ya digidigi wa thamani ya Sh583,750,” amesema Kamanda Katabazi.
Kamanda Katabazi amesema uhalifu wa sasa hauangalii jinsia ya mtu badala yake matukio hayo sasa yamekuwa yakifanywa na makundi yote na kuwataka wananchi kuacha tabia hiyo mara moja kwani ni kinyume cha sheria.