NA MWANDISHI WETU, ZANZIBAR
ALIYEKUWA Askari Polisi FFU, Ramadhani Ali maarufu Afande Rama, amefikishwa katika Mahakama ya Mkoa wa Vuga, kujibu mashtaka mawili yanayomkabili.
Mbele ya Hakimu Khamis Ali Simai, Mwendesha Mashtaka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar, Muhammed Saleh, alidai mahakamani kuwa mshtakiwa anakabiliwa na mashtaka mawili ambayo ni kuruhusu kuingiliwa kinyume na maumbile na kufanya maudhui makubwa ya kingono.
Alidai kuwa mshtakiwa alitenda makosa hayo mapema Machi mwaka huu, kitendo ambacho ni kosa kwa mujibu wa Sheria za Zanzibar.
Mshtakiwa huyo alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza akitokea mahabusu ya polisi bila ya wakili wa kumsimamia.
Shtaka hilo limeahirishwa hadi Aprili 4, mwaka huu na mshtakiwa amepelekwa mahabusu huku upande wa mashtaka ukidai unaendelea na upelelezi.
Ilidaiwa kuwa askari huyo alijihusisha na mapenzi ya jinsia moja kwa kuruhusu kuingiliwa kinyume na maumbile huku video fupi inayoonesha tukio hilo ikisambaa mtandaoni.
Hivi karibuni, Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Hamad Hamad, alisema askari huyo alishapandishwa kwenye mahakama ya kijeshi kutokana na tuhuma hizo ambazo ni kinyume na mwongozo na kanuni za kiutendaji wa jeshi hilo (PGO).