NA MWANDISHI MAALUM, KINSHASA
MKUTANO wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) umehitimishwa jijini Kinshasa Machi 19 , 2023, huku ajenda za kujikwamua kiuchumi katika kanda hiyo ya Kusini mwa Afrika zikipewa kipaumbele
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo unaotathmini utekelezaji wa mipango ya Mwaka wa Fedha 2022/2023 na kuweka mikakati ya utekelezaji wa mipango ya Mwaka wa Fedha 2023/2024, umeongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Stergomena Tax akisaidiana na Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde
Maeneo ambayo Waziri Tax alichangia wakati taarifa za utekeleaji zilipokuwa zinawasilishwa ni pamoja na hatua iliyofikiwa kuhusu tafsiri ya nyaraka muhimu za SADC katika lugha ya Kiswahili, ujenzi wa Sanamu la Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Mpango wa Kanda wa ununuzi wa pamoja wa vifaa vya afya unaoratibiwa na Bohari Kuu ya Dawa (MSD).
Waziri Tax alisisitiza umuhimu wa kuongeza kasi katika utekelezaji wa maeneo hayo, kufuatia maelezo kuwa utekelezaji wa tafsiri ya nyaraka muhimu za SADC katika lugha ya Kiswahili upo katika hatua za kumpata mzabuni wa kufanya kazi hiyo na ujenzi wa Sanamu la Baba wa Taifa unaendelea, na kazi hiyo inatakiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka 2023.
Kuhusu Mpango wa Kanda wa ununuzi wa pamoja wa vifaa vya afya, Dk.Tax amesema MSD inaendelea na jukumu hilo na kutoa wito kwa nchi wanachama kuongeza kasi ya kuitumia bohari hiyo ya dawa kwa kuwa manufaa yake ni makubwa hususan katika kupunguza gharama za ununuzi wa dawa na vifaa tiba.
Awali, wakati wa hafla ya ufunguzi, hotuba za viongozi ikiwa ni pamoja na; Waziri Mkuu wa DRC, Jean-Michel Nyenge; Waziri wa Mtangamano wa Kikanda wa DRC na Mwenyekiti wa Mkutano huo, Didier Mazenga Mukanzu na Katibu Mtendaji wa SADC, Elias Magosi ziliainisha maeneo muhimu ya kuwekewa mkazo ili kupanua wigo wa mtangamano na kuongeza kasi ya maendeleo baina ya nchi wanachama.
Maeneo hayo ni pamoja ujenzi wa miundombinu, ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani ya bidhaa za madini, ngozi na kilimo, kuwa na nishati ya umeme ya uhakika, usawa wa kijinsia katika siasa na zaidi ya yote ni umuhimu wa kuimarisha amani na usalama katika kanda.
Ilielezwa kuwa maeneo hayo yameainishwa vyema katika Mpango Mkakati wa Maendeleo wa Kanda (2020-2030) ambapo Sekretarieti ya SADC imeahidi kuendelea kuratibu na kuhamasisha utekelezaji wake.
Kwa upande wa Tanzania, miradi 11 imeingia katika mpango huo ambayo inahusu uendelezaji wa sekta ya maji katika mto Songwe, usindikaji wa ngozi, uzalishaji wa mbolea, uchumi wa buluu, nishati, utafiti,, elimu na utengenezaji wa dawa za binadamu na wanyama.
Tanzania imejipanga kutekeleza miradi hiyo hasa ya nishati na uzalishaji wa mbolea ili iweze kuuza katika nchi wanachama ambazo nyingi zinakabiliwa na uhaba wa nishati ya umeme na mbolea.