NA MWANDISHI WETU, DODOMA
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Wakuu wa Wilaya nchini wakasimamie ajenda za kitaifa ikiwemo ya mapambano dhidi ya rushwa.
Amewataka pia wasimamie changamoto za upatikanaji wa ajira, kudhibiti vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto, kusimamia uoto wa asili na kusuluhisha migogoro ya wakulima na wafugaji. Mengine ni usimamizi wa miradi ya maendeleo, ukusanyaji wa mapato ya Serikali na utatuzi wa kero za wananchi.
Ametoa wito huo leo mchana (Jumamosi, Machi 18, 2023) wakati akifunga Mafunzo ya Uongozi kwa Wakuu wa Wilaya 138 yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Mtakatifu Gasper, jijini Dodoma.
Waziri Mkuu Majaliwa amesema: “Katika kukabiliana na tatizo la rushwa, nendeni mkakemee na kufuatilia mianya ya rushwa ili izibwe na kuhakikisha wananchi wanapata huduma muhimu bila kulazimishwa kutoa rushwa.”
Akiwakumbusha wajibu wao, Waziri Mkuu amewataka wakuu hao wa wilaya wafuate maagizo na maelekezo ya mamlaka iliyowateua na akawataka watambue kuwa wao ni wawakilishi wa Mheshimiwa Rais kwenye maeneo yao.
“Aina ya utumishi huu wa uteuzi ni tofauti na ule wa mchakato wa interview. Kwa hiyo mnapaswa kutambua mwenye mamlaka anataka nini, mnapaswa kuenenda na maono yake, matakwa yake na maelekezo yake,” amesisitiza.
“Ili mradi umeteuliwa na umeapa, wewe ni kiongozi wa Serikali wa eneo ulilopewa na ni msimamizi wa shughuli zote za Serikali na hata za sekta binafsi. Kwa hiyo unalo jukumu la kufuatilia na kujiridhisha je, yanayofanywa na sekta binafsi yanalenga kuleta maendeleo?” amesisitiza.
Akielezea umuhimu wa majukumu yao, Waziri Mkuu amesema: “Tunapozungumzia maendeleo ya nchi, hatuwezi kuyafikia bila uwepo wenu kwa sababu ninyi ndiyo wenye watu. Kuna wilaya ina Halmshauri moja nyingine mbili au tatu. Ni lazima ufuatilie yanayoendelea katika wilaya yako na matarajio ya Mheshimiwa Rais ni kuona kuwa mtawahudumia wananchi, mtawatumikia na kusikiliza kero zao.”
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na wakuu hao wa wilaya, Waziri wa Nchi (OR-TAMISEMI), Angellah Kairuki alisema mafunzo hayo ya siku sita yaliyoanza Machi 13, mwaka huu yalihusisha washiriki 139 ambapo kati yao 37 ni wapya na wengine 102 ni wale wanaoendelea na nyadhifa zao.
Akitoa rai kwa washiriki hao, Waziri Kairuki alisema: “Baada ya kupata mafunzo haya, tunataraji mkirudi kwenye vituo vyenu vya kazi, mtatekeleza yale yote mliyoyapata kwa kushirikiana na wengine ili kuharakisha utekelezaji wa shughuli za Serikali.”
Mafunzo hayo yaliyoendeshwa na Taasisi ya Uongozi, yalihusisha mada 17 zilizogusa masuala mbalimbali ambapo baadhi ya Mawaziri walishiriki kutoa ma