NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
MAREKANI imeahidi kuendelea kuiunga mkono Tanzania katika jitihada zake za kuimarisha uchumi wake na maendeleo ya wananchi kwa kutoa fedha na ujuzi mbalimbali pamoja na kuvutia uwekezaji kupitia ubia kati ya sekta ya Umma na Binafsi.
Ahadi hiyo imetolewa na Balozi mpya wa Marekani nchini Tanzania, Michael Battle, alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango Dk Mwigulu Nchemba, katika Ofisi Ndogo za Wizara hiyo, jijini Dar es Salaam, alipofika kujitambulisha.
Battle amepongeza hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali katika kusimamia na kukuza uchumi wa nchi na kuamua kuwekeza kiasi kikubwa cha fedha katika Bajeti yake kwenye sekta za uzalishaji zinazogusa maisha ya watu, kikiwemo kilimo.
“Tunaahidi kuwa Marekani itaendelea kuiunga mkono Serikali ya Kiongozi shupavu ambaye situ kwamba anapigania sana maisha ya watanzania, lakini pia amekuwa mwanadiplomasia anayepigania maendeleo na utangamano wa Afrika” amesema Battle.
Battle amesema kuwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amegusa mioyo ya wamarekani na viongozi wake ndiyo sababu za Makamu wa Rais wa Marekani Kamara Harris kupanga ziara ya kuitembelea Tanzania ambapo viongozi hao wawili watafungua fursa zaidi za ushirikiano wa kiuchumi na kijamii.
Kwa upande wake, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Nchemba, ameahidi kufikisha ujumbe wa Balozi huyo kwa Rais Samia , Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kumwahidi kiongozi huyo kwamba Tanzania ipo tayari kutumia fursa za ushirikiano wa nchi hizo mbili kuwahudumia watanzania.
Ameiomba Marekani kupitia Shirika lake na Maendeleo la Kimataifa (USAID), kuhakikisha kuwa inazipa kipaumbele Asasi zisizo za Kiserikali (AZAKI) katika utekelezaji wa program zake mbalimbali hapa nchini kwa kuzijengea uwezo wa kifedha na kiuendeshaji badala ya kufadhili Taasisi za nje pekee zinazopewa fedha kutekeleza miradi hiyo badala ya kuzinufaisha AZAKI za hapa nchni.
Kuhusu uamuzi wa Serikali wa kuzipa kipaumbele sekta za uzalishaji katika mgao wa fedha za Bajeti, Dk. Nchemba alisema kuwa sekta hizo ikiwemo kilimo, mifugo, uvuvi, uendelezaji wa wafanyabiashara wadogo (Machinga), utakuza uzalishaji wa mazao, lakini pia kuongeza ajira kwa wananchi hususan vijana.
Naye Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID) Kate Somvongsiri, amemshukuru Dk. Nchemba kwa kutoa hoja ya Taasisi za wazawa zikiwemo AZAKI, kupewa kipaumbele katika miradi inayotekelezwa kupitia Shirika lake hapa nchini.
Amesema kuwa utaratibu uliopo hivi sasa ni kwamba asilimia 25 ya rasilimali zinazotumika na Shirika lake katika nchi zinaelekezwa kwenye taasisi za wazawa na kwamba kiwango hicho kitaendelea kuongezeka wakati unapowadia kufanya hivyo lakini lengo ni kufika asilimia 50.
Ushirikiano wa Tanzania na Marekani umetimiza zaidi ya miaka 50 ambapo makubaliano ya kwanza ya kuanzishwa kwa uhusiano huo yalisainiwa mwaka 1968.