NA EDNA BONDO, DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye ametoa wito kwa watu kujenga utaratibu wa kusoma vitabu.
Sambamba na hilo Waziri Nape ametoa hamasa kwa watu kuandika vitabu.
Hayo yameelezwa na Waziri Nape katika Uzinduzi wa Kitabu cha Mwanahabari na Mtumishi wa Mungu Lillian Mwasha kiitwacho Darling Listen uliofanyika usiku wa Machi 17, 2023 jijini Dar es salaam.
Waziri Nape amesema anafurahia uwepo wake katika uzinduzi huo kwani anaamini kila kitu ni mpango wa Mungu.
“Nimefurahi jioni ya leo kuwepo mahali hapa, wakati Lilian ananiambia juu ya jambo lake niliona siwezi..lakini aliniambia Mheshimiwa Waziri utafanya na imekuwa..niwahakikishie hakuna hata mmoja aliyepo mahali hapa amekuja kwa bahati mbaya..kila kitu ni mpango wa Mungu” amesema Waziri Nape
Amesema kitendo kilichofanywa na Mwasha ni cha kijasiri sana na ametumia nafasi hiyo kumpongeza Mwanahabari huyo kwa hatua hiyo.
Aidha Waziri Nape amewataka watanzania kukiri na kupokea yaliyo mema katika maisha yao, familia zao na Taifa kwa ujumla.
Katika hatua nyingine Waziri Nape alimpongeza Mkurugenzi wa Kituo cha Redio na Runinga cha Efm na tVe Francis Ciza kwa kujitia kwake kudhamini uzinduzi wa Kitabu cha Darling Listen .
Pia Waziri Nape alimpongeza Mkurugenzi huyo kwa kukubali kuanzisha kipindi maalum cha ibada kiitwacho Church on Fire ambacho kitazinduliwa na kuanza hivi karibuni ambacho kitakuwa kikirushwa na TVe huku kikiongozwa na Mchungaji Emmanuel Mgaya (Masanja Mkandamizaji) Mchungaji Richard Hananja na Lillian Mwasha.
Kwa upande wake Mwasha aliwashukuru watu wote waliohudhuria uzinduzi wa kirabu chake na kusisitiza kuwa amebarikiwa sana.