NA TATU MOHAMED, DAR ES SALAAM
SHIRIKA la Maendeleo la Kimataifa la Japani (JICA) limerejesha Mpango wa Kujitolea wa Japan (JOCV) baada ya kusimama kwa takriban miaka mitatu kutokana na janga la UVIKO-19.
Katika kurejesha huduma hiyo, Mhandisi wa Mitambo wa kujitolewa aliwasili nchini Februari 7, 2023 na kupangiwa kazi katika vituo cha Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) ili kutekeleza mpango huo.
Katika taarifa iliyotolewa kwa nyombo vya habari na Mshauri Mkuu wa JICA, Raymond Msoffe, imeeleza kuwa kwa sasa mfanyakazi huyo anafanya mafunzo ya lugha ya Kiswahili na utamaduni kwa mwezi mmoja kabla ya kuanza kazi yake mwezi huu.
“Muda mfupi kabla ya janga la kimataifa la UVIKO-19 kutokea Machi 2020, jumla ya wafanyakazi wa kujitolea 60 wa JICA wa nyanja mbalimbali nchini Tanzania, walitakiwa kurejea Japan jambo ambalo halikutarajiwa,” amesema Msoffe.
Ameongeza kuwa, wakati huo wafanyakazi wa kujitolea wa JICA walikuwa karibu kuondoka Japan kuelekea Tanzania Machi 2020, lakini matumaini yao yalikatishwa na janga hilo.
“Alikuwa anasubiri kuja Tanzania kwa takribani miaka mitatu na sasa ndoto yake imetimia. Mjapani huyu anaishukuru Serikali ya Tanzania kwa kumkubali kufanya kazi ya kubadilishana maarifa na ujuzi wake na Watanzania,” alisema Msoffe.
Mpango wa JOCV ni mojawapo ya Mipango ya ushirikiano wa kiufundi wa Japan inayoendeshwa kama sehemu ya Misaada Rasmi ya Maendeleo (ODA) inayotolewa kusaidi nchi na majimbo yapatayo 98 ikiwa ni pamoja na Tanzania.
Lengo kuu ni kushirikiana katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii, kubadilishana maarifa na utaalamu wa kiufundi wa Japan katika nchi zinazoendelea na kuimarisha urafiki.