NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
SHEIKH Said Ukatule(80) aliyekuwa mahabusu ya Gereza Kuu la Ukonga, jijini Dar es Salaam, alipokuwa akishikiliwa na serikali kwa mashtaka ya ugaidi, amefariki dunia ghafla mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu, Salma Maghimbi.
Taarifa iliyotolewa Jumanne Machi 07, 2023 na Katibu Mkuu wa Shuraa ya Maimamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda, zinaeleza kuwa Sheikh Ulatule, alifariki dunia mbele ya Jaji huyo Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masijala Kuu ya Dar es Salaam, Machi 04, 2023.
Kabla ya kukutwa na mauti, Sheikh Ulatule alikuwa akijaribu kumueleza Jaji Maghimbi, matatizo wanayopitia wafungwa na mahabusu katika gereza hilo.
“Tarehe 4 Machi 2023, Jaji Magimbi alifanya ziara katika Gereza la Ukonga, baada ya kuwasikiliza wafungwa iliwadia zamu ya mahabusu wakiwamo waislamu wanaotuhumiwa kufanya vitendo vya ugaidi.”
“Katika kikao hicho, Sheikh Ulatule aliinua mkono na Jaji Maghimbi alimpa fursa ya kueleza shida zake, hata hivyo hakuweza kusema lolote bali alianguka na kufariki dunia papo hapo mbele ya Jaji, wafungwa, mahabusu na maofisa wa Magereza,” imeeleza taarifa ya Sheikh Ponda.