NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
TAKWIMU za kidunia zinaonesha kwamba ushiriki wa wanawake katika masuala ya teknolojia ni mdogo ikilinganishwa na wanaume na kwamba hali hiyo inasababishwa na changamoto ya usalama mitandaoni.
Kauli hiyo imetolewa leo Machi 07, 2023 jijini Dar es Salaam na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye wakati akifungua kongamano maalum la wanawake na teknolojia lililoandaliwa na Shirika lisilokuwa la Kiserikali la The LaunchPad Tanzania.
Nape amesema zipo jitihada kadhaa zinazofanyika ili kuongeza idadi ya ushiriki wa wanawake katika sekta hiyo ya teknolojia ikiwemo ya Serikali kuwa tayari kupokea maoni kutoka kwa wadau kuhakikisha mtandao unakuwa salama.
“Takwimu za dunia zinaonesha idadi ya wanawake na vijana hasa wanawake wanaoshiriki kwenye shughuli zinazotokana na TEHAMA sio nzuri kwani idadi ni mdogo ukilinganisha na wanaume lakini zipo jitihada zilizokuwa zinafanyika kuona namna ya kuongeza idadi ya ushiriki wao,” amesema.
Amesema ni ukweli ulio wazi kuwa waathirika wakubwa wa nyanyasaji mitandaoni ni wanawake hivyo kama Serikali wanawajibu wa kuchukua hatua kali ikiwemo ya kutunga sheria kadhaa ikiwemo ya kulinda taarifa binafsi kwa lengo la kuhakikisha mtandao upo salama ili kuwavutia wanawake kushiriki.
Nape amesema nchini takwimu zinaonesha zaidi ya asilimia 51 ya idadi ya watu ni wanawake hivyo wasiposhiriki vya kutosha jamii kubwa ya Tanzania itakuwa haijashiriki katika Tehama.
“Tafiti zinaonesha wanawake wapo makini kwenye shughuli zao hivyo tukiwahamasisha wakashiriki katika masuala ya teknolojia kwa sehemu kubwa mapinduzi makubwa ya kiuchumi katika jamii yetu yatapatikana, ” amesema Nape nakuongeza
“Rais Samia Suluhu Hassan anawahakikishia kuwa Serikali ipo tayari kupokea maoni na ushauri wa wadau wengine katika kuhakikisha mtandao upo salama na kuwa eneo zuri la watu kufanya shughuli zao na kuhakikisha idadi ya wanawake inaongezeka katika matumizi ya mtandao ili waweze kufanya shughuli zao za kila siku,” ameeleza.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi isiyo ya kiserikali la The LaunchPad Tanzania, Carol Ndosi amesema kongamano hilo limejikita kufanya tathmini kama nchi imefikia wapi katika safari ya wanawake na teknolojia, kuangalia fursa na changamoto wanazokutana nazo.

“Tumegundua takwimu tofauti tofauti ambazo zinaonesha kuwepo na mwanya mkubwa katika matumizi na kutengeneza teknolojia ambapo wanawake ni wachache na hawafahamiki,” amesema.
Amesema kupitia kongamano hilo wameiomba wizara husika kuangalia sera ya ICT kutokuwepo na kipengele kilichotaja wanawake, kupitia sheria itakayotoa uhakika wa usalama mtandao kwa wanawake ili kuweza kuhamasisha ushiriki wao.
Naye Mshiriki wa kongamano hilo, Mhandisi Fatuma Mwamba aliiomba serikali kuyafanyia kazi mambo watakayojadiliana na kuyaingiza katika sera ya Tehama.