NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
WIZARA ya Fedha na Mipango imekanusha taarifa inayosambaa mitandaoni ikidai kuwa Benki ya Uwekezaji ya Ulaya( EIB) inaidai Tazania dola za Kimarekani bilioni 4.1 (zaidi ya shilingi trilioni 10 za Kitanzania) na kwamba mwezi Januari, Waziri wa Fedha Dk Mwigulu Nchemba, aliomba mkopo mwingine kwenye Benki hiyo, lakini ilikataa kutoa mkopo huo kwa sababu haijalipwa deni kwa muda wa miezi 28.
Kwa mujibu wa Taarifa ya Wizara iliyotolewa na Idara ya Mawasiliano ya Wizara hiyo Machi 05, 2023,mara kwa mara, Mtandao wa kijamii wa Tanzania Abroad TV (TAT), umekuwa ukitoa taarifa za uzushi, upotoshaji na uzandiki dhidi ya Wizara ya Fedha na Mipango na Serikali kwa ujumla huku lengo lake likiwa halifahamiki .
“Tunawaomba watanzania na Jumuiya ya Kimataifa, mzipuuze taarifa hizo, ambazo hazina ukweli wowote na kwa vyovyote vile zinalenga kupotosha umma na kuleta taharuki isiyokuwa na sababu za msingi.Pamoja na kwamba EIB ni mdau mkubwa wa maendeleo na ina uhusiano mzuri na nchi yetu pamoja na Sekta binafsi kwa muda mrefu na ina uhusiano mzuri na nchi yetu kwa ujumla, Serikali haina mkopo wa kiasi hicho kilichotajwa kutoka katika Benki hiyo” ilifafanua taarifa hiyo na kuongeza
“Tunapenda kuwakumbusha wamiliki na watoa habari katika mitandao ya kijamii kwamba ni kosa kisheria kutoa taarifa za upotoshaji, uzandiki na uzushi kwa mujibu wa Sheria ya Huduma ya Vyombo vya Habari (2016). Hivyo Tunatoa onyo kwa mtandao wa kijamii wa TAT na watu wengine wanaoeneza taarifa za namna hiyo mitandaoni kuhusu Wizara ya Fedha na Mipango, na kuchafua taswira nzuri ya Wizara na Serikali katika jamii, kuacha tabia hiyo mara moja.”