NA MWANDISHI WETU, NJOMBE
WAZIRI wa Kilimo, Hussein Bashe ameagiza kukamatwa kwa Meneja Masoko wa Kampuni ya Mbolea ya Minjingu Mkoa wa Njombe, Dk Mshindo Msolla, msimamizi wa ghala la Minjingu na meneja wa Kanda Nyanda za Juu Kusini na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Michael Sanga kwa tuhuma za kukutwa na mifuko 776 ya mchanga kwenye ghala la mbolea la kampuni hiyo inayodhaniwa huenda inatumika katika kuchakachua mbolea na kuuzwa kwa wananchi.
Bashe ametoa agizo hilo leo Jumapili Machi 5, 2023 wakati akizungumza kwa njia ya simu mara baada ya kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa wa Njombe kufanya ukaguzi katika ghala hilo lililopo mkoani Njombe.
Amesema licha ya TFRA kuipiga faini ya Sh30 milioni kampuni hiyo lakini yeye taarifa hiyo hakupewa zaidi ya kuipata kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka hivyo awekwe ndani na kutoa maelezo.
Amesema pamoja na kuagiza kuwekwa ndani kwa watu hao lakini uchunguzi sahihi unatakiwa kuendelea kufanyika na baadaye atatoa maelekezo.
“Kwasababu haiwezekani kuwa na mifuko ya michanga na hatujui wakulima wangapi wamepewa mifuko ya michanga” amesema Bashe.
Amesema meneja wa kampuni hiyo naye anatakiwa kukamatwa na kutoa maelezo kwakuwa haiwezekani ghala kukutwa na mchanga halafu wao wasiwe na taarifa.
Ameagiza TFRA kutoa taarifa ya idadi ya wakulima mkoani Njombe ambao wametumia mbolea ya Minjingu ili wakatembele huenda walinunua mifuko ya mchanga.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka amesema serikali ya mkoa inawapa pole wakulima ambao wamekumbwa na kadhia hiyo kwa namna yoyote kwa kuwa watakuwa wamepata mbolea ambayo siyo matarajio yao.
Amesema hilo pia sio kusudio la Rais Samia alilokusudia kwamba wananchi ambao wanafanya kilimo waweze kupata unafuu wa mbolea.
“Sisi kama mkoa tuwaombe sana wafanyabiashara kwenye eneo la mbolea wazingatie uaminifu, uadilifu, utaifa na uzalendo” amesema Mtaka.
Amesema shughuli ya kilimo kwa sehemu kubwa ya nchi inafanywa na watu wa hali ya chini sana bado wanajikokota kwenye jembe la mkono na ng’ombe na siyo mtu mwenye mtaji mkubwa hivyo analima akitegemea hicho ni chakula chake cha msimu mzima.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi mkoni hapo, Deo Sanga amesema chama hicho kimepokea taarifa hiyo kwa masikitiko kutokana na hicho kinachoendelea katika suala la mbolea.
Amesema mbolea ya ruzuku imeletwa ili kupunguza gharama ambazo zilikuwepo na kuuzwa Sh130,000 hadi Sh140,000 ili wakula wapate nafuu baada ya kuuzwa Sh.70,000.
“Sisi kama chama tumepokea kwa masikitiko na mkuu wa mkoa ufuatilie tutashirikiana pamoja kuona wakulima wangapi ambao wamenunua mbolea ya mchanga.” amesema Sanga.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Hamisi Issah amesema amepokea maelekezo ya kuwakamata wahusika ili kutoa maelezo na hatua zingine ziweze kufuatwa.
“Kwahiyo maelekezo tunaendelea nayo sampo zimechukuliwa kwa ajili ya uchunguzi na mambo mengine yataendelea.” amesema Issah.
Meneja Masoko wa kampuni ya mbolea ya Minjingu Dk Mshindo Msolla amesema mfanyakazi aliyefanya tukio hilo hayupo lakini suala hilo tayari walishalipeleka polisi atafutwe na wao wapo tayari kutoa ushirikiano.
“Huyu akipatikana atakuwa tayari ameshatoa suluhisho sisi kama kampuni hili jambo limetudhangaza na hatukulitegemea” amesema Dk Msolla.