NA DENIS SINKONDE, SONGWE
BAADA ya wananchi wa Kijiji Cha Ndolezi Kata ya Mlangali wilayani Mbozi mkoani hapa kuiomba Serikali kuwalipa fidia, serikali kupitia kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurungezi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro(NCAA) Venance Mabeyo amesema wanatarajia kuwalipa wananchi wote waliothaminisha maeneo yao bila kuchelewa.
Jenerali Mabeyo ametoa kauli hiyo Machi 4,2023 wakati akizindua Makumbusho yaliyopo katika kitongoji Cha Isela Kijiji Cha Ndolezi kata ya Mlangali wilayani Mbozi.
Jenerali Mabeyo amesema serikali imekusudia kulipa fidia Kwa wananchi kwenye kaya 176 shilingi bilioni 1.4 ili wakajenge makazi mapya na kuacha eneo la makumbusho ya kimondo likiendelezwa na amewapongeza wananchi wanaoishi katika eneo hilo kwa kukubali kutoa ardhi yao kwa ajili ya kuendeleza eneo hilo kiutalii.
“Serikali imekusudia kulipa Bil. 1.4 kwa wananchi waliopisha upanuzi wa kituo hiki hivyo naomba muendelee kuipenda selikali yenu kwa vile hadi sasa tumeshatenga kiasi cha fedha cha kuanza kulipa fidia hizo” amesisitiza Mabeyo
Katika hotuba yake Jenerali Mabeyo amefafanua kuwa moja ya shabaha ya Serikali ya kuzindua Makumbusho hayo ni kuhakikisha fursa za kiuchumi zinatapakaa kila pembe ya nchi ili kuwawezesha wananchi kujikwamua kiuchumi kupitia sekta ya utalii.
Vile vile Mwenyekiti huyo ametumia fursa hiyo kuwashukuru viongozi wa kimila kwa kutoa ushirikiano kuonesha mila na desturi ya jamii inayokaa katika maeneo hayo na kusema kuwa Makumbusho hiyo ni ya kwanza ya aina yake kwa Nyanda za Juu Kusini.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Songwe Dk Francis Michael amewataka NCAA kuendelea kufanya maboresho zaidi katika kituo hicho cha Kimondo ili kuwavutia watalii wengi kutembelea eneo hilo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi George Msyani amemuomba mwenyekiti wa NCAA Jenerali Mabeyo kusimamia na kuweka msukumo wa haraka kulipwa fidia hiyo kwani kutolipwa Kwa wakati wananchi hao kunaleta sura ya kudhulumiwa na hivyo kuichukia serikali.
Hata hivyo licha ya tamko la kulipwa fidia baadhi ya wananchi wameiomba serikali iwatengee maeneo maalumu ya kujenga makazi yao mapya huku wakidai kulipwa fidia bila kuwapa maeneo ya kujenga itakuwa sio kuwatendea haki.