NA MWANDISHI WETU
SHIRIKISHO la soka nchini (TFF) limemtangaza Adel Amrouche mwenye asili ya Algeria kuwa Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ ambaye anajua kuzungumza Kiswahili hali inayoaminiwa ataweza kuwasiliana vema na wachezaji wa Kitanzania.
Taarifa ambayo imetolewa leo Machi 4,2023 na TFF, imeeleza kuwa kocha huyo raia wa Ubelgiji ana uzoefu katika soka kwa kuzifundisha timu kadhaa za taifa katika ukanda wa Kusini, Mashariki, Kati na Kaskazini.
Imeelezwa kuwa kocha kocha huyo amewahi kutwaa tuzo ya Kocha Bora, Afrika Mashariki mwaka wa 2013, baada ya kuipa ubingwa wa Cecafa timu ya Taifa ya Kenya. Aliwahi pia kucheza michezo 20 bila kupoteza.
Kwa nyakati tofauti kocha huyo amewahi kuzifundisha timu za Yemen, Libya, Burundi, Equatorial Guinea, Botswana. Pia aliwahi kuifundisha klabu ya Motema Pembe ya DR Congo.
Pia taarifa zinasema kocha huyo atakiwa kilipwa mshahara na Serikali jambo ambalo litaipunguzia mzigo TFF katika suala la kulipa mshahara.
Tofauti na Kiswahili kocha huyo anajua kuzungumza Kiarabu, Kifaransa, Kingereza na kwa nyakati tofauti aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Ufundi kwenye michezo katika klabu za Ubelgji na Ukraine, Pia kocha huyo ana shahada ya uzamili katika kuwasoma watu katioka utimamu.
Sifa nyingine kwa kocha huyo ni Mkufunzi wa walimu wa Pro Licence wa Shirikisho la Soka la Ulaya UEFA na amefanikiwa kuzalisha makocha lukuki, bora barani Afrika na anauzofu na soka la vijana na ndio kazi aliyoifanya kwa zaidi ya mika 10 nchini Ubelgiji na Algeria